Viti Maalumu Ukawa sikio la kufa

23Jun 2016
Salome Kitomari
Dodoma
Nipashe
Viti Maalumu Ukawa sikio la kufa

MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Theonest, ambaye jana alimaliza adhabu ya kutohudhuria vikao vitatu vya Bunge kwa kosa la kusema uongo bungeni,

Mbunge wa ulanga (CCM) Goodluck Mlinga.picha milladayo.com

Aamejikuta matatani tena baada ya kumvua baraghashia Goodluck Mlinga (CCM),Mbunge wa Ulanga wakati wakitoka nje ya ukumbi huo kama ilivyo kawaida ya wapinzani.

Mbunge huyo jana alimaliza kutumikia adhabu ya kutohudhuria vikao vitatu kwa kosa la kusema uongo bungeni dhidi ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, kuwa akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alidhulumu viwanja vya wakazi wa mabondeni.

Naibu Spika alitoa adhabu hiyo wiki iliyopita ambayo iliambatana na kulipwa nusu mshahara na posho, lakini jana alidaiwa kumvua baraghashea Mlinga na kutokomea nayo nje ya ukumbi.

Kufanyika kwa kitendo hicho kulifichuliwa na Mlinga baada ya kuomba mwongozo wa Spika.

Katika ombi hilo, Mlinga ambaye aliwahi kudai ndani ya Bunge kuwa Viti Maalumu upande wa upinzani huwa hawapati nafasi hizo bila ya kutoa rushwa ya ngono kwenye vyama vyao, aliorodhesha hoja sita katika mwongozo alioomba.

Miongoni mwa hoja hizo ni Anatropia kamvunjia heshima mke wake na wananachi wa Ulanga.

Alisema kuvuliwa kofia hiyo kulimpoteza sifa ya kuwakilisha wananchi wake bungeni kwa muda huo kwa kuwa kanuni inataka avae baraghashia pamoja na kanzu.

“Kwa mujibu wa vazi hili na utamaduni wake anayetakiwa kunivua ni mke wangu wa ndoa," alisema Mlinga.

Mlinga ambaye alifuta kauli yake Mei baada ya kutakiwa kufanya hivyo na kiti cha Spika, alisema kitendo cha Anatropia pia kimeingilia kwa nguvu himaya ya mke wake wakati "amari ya Mungu kwa dini zote (inasema) usitamani mali ya mtu mwingine."

"Hivyo ametamani mume wa mtu mwingine.”

Mlinga alisema Mbunge huyo amevunja msimamo wa chama chake wa kutowajongelea wabunge wa CCM.

Dk. Tulia Ackson alitaka ufafanuzi kama amevuliwa akiwa ndani ya Bunge ndipo mbunge huyo aliposema “Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha ajabu sana. Amenivua nikiwa ndani ya bunge hili, nikiwa nimekaa kwenye kiti.”

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika huyo alisema atafuatilia kujua ukweli wake na kutoa ufafanuzi unaotakiwa.

Habari Kubwa