Vituo viwili vya yatima vyapokea michango ya Ramadhan

15May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Vituo viwili vya yatima vyapokea michango ya Ramadhan

Ni ada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan kutoa sadaka na kuwasaidia maskini.Kwa kuzingatia maelekezo hayo ikiwa pia ni kawaida ya utaratibu wake, kampuni ya QNET imetoa misaada mbali mbali kwa vituo viwili vya watoto yatima Jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Michango hiyo imetolewa ikiwa kama sehemu ya kuadhimisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Kwa upande wa Tanzania Bara, QNET imetoa misaada kwenda kwenye kituo cha watoto yatima Kigamboni, Dar es Salaam.

Kituo hicho kinaitwa Safina Widow and Child Care Foundation na kwa upande wa tanzania visiwani, mchango ulienda kwenye kituo cha Takrim Foundation.

Kituo cha Kigamboni kilianzishwa 2007 kikiwa na watoto 10 tu. Kituo hicho cha watoto yatima sasa kina makazi ya yatima zaidi ya 50 wanaoishi na kusoma huku wakiishi katika kituo hicho. 

Akitoa maoni yake, Athumani Juma ambaye ni Mlezi Msaidizi wa kiuo hicho alisema msaada huo una umuhimu mkubwa katika kuchangia malezi ya watoto hao.

Msimamizi huyo aliendelea kusema kuwa michango hiyo itawasaidia kutimiza mahitaji yao ya msingi. Alisema kuwa michango hiyo imekuja wakati muafaka na itapunguza gharama zao za uendeshaji.

“Hii itatuwezesha kuelekeza fedha hizi kwenye mahitaji mengine ya kituo,” alisema Juma

Kwa upande wa Zanzibar, Visiwani, kituo cha Takrim Foundation kinacho walea yatima zaidi ya 90 kupitia mfumo wa huduma ya nyumbani, nacho kilipokea michango kutoka kwa kampuni ya QNET.

Mfumo unaotumiwa na kituo hicho visiwani zanzibar ni mfumo tofauti na unaotumiwa na vituo vya tanzania bara.

Katika mfumo wao watoto yatima wanaishi katika nyumba za walezi wa kujitolea ili waweze kua katika mazingira ya kinyumbani badala ya kulelewa kwenye kituo maalumu kama wenzao wa Bara. 

Kituo hicho kilianzishwa mnamo wa 2020 na kimesajiliwa mapema mwaka huu na kinalea yatima na watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu au wasio na makazi rasmi.

Zaidi ya mahitaji yao ya kimsingi ya kila siku, kituo hicho kinahakikisha watoto wanakua katika mazingira bora katika familia za walezi wakujitolea.

Pamoja na mambo mengine, QNET ilitoa msaada wa magodoro 10, mchele kilo 100, sukari kilo 100 magunia 5 ya unga wa ngano na magunia 10 ya unga wa mahindi.

Vitu vingine ni pamoja na magunia matatu ya mkaa, maboksi mawili ya pedi za kike, ndoo tatu za mafuta ya kula, ndoo mbili za maziwa ya unga, magunia mawili ya sabuni ya unga, masanduku mawili ya sabuni ya kuogea, dawa mbili za meno, dazeni 17 za vitabu, maboksi 10 ya kalamu, maboksi tano ya penseli na maboksi mawili ya karatasi.

Habari Kubwa