Vituo vya malezi suluhisho mmomonyoko maadili kwa watoto

21Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Vituo vya malezi suluhisho mmomonyoko maadili kwa watoto

IMEELEZWA Vituo vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika jamii ndio suluhisho la kero mbalimbali  zinazojitokeza ikiwamo mmomonyoko wa maadili kwa watoto.

Hali hiyo imeisukuma  serikali kuanzisha mradi wa ujenzi wa vituo hivyo unaochangiwa na wananchi wa maeneo husika.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Sebastian Kitiku ameyasema hayo leo alipokagua  ujenzi wa vituo hivyo katika Halmashauri za wilaya nne zilizopo mkoani Dodoma.

Kitiku amesema Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamaii iliona umuhimu wa vituo hivyo  ili kusaidia wazazi na walezi katika maeneo  husika kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi huku wakiwa na uhakika wa malezi ya watoto wao.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa vituo hivyo vitamilikiwa na kusimamiwa jamii na husika ambayo pia itakuwa na jukumu la kuanzisha vikundi vya malezi kwa lengo la kuiwezesha jamii kuwa na malezi Chanya kwa watoto.

"Hivi Vituo vitatusaidia katika kutoa elimu ya malezi kwa wazazi na watoto pia kwani vikundi vya malezi vya wazazi vitaanzishwa ili kuendana na uendeshaji wa Vituo hivi" amesema

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kogwa, Dk. Omary Nkulo amesema vituo hivyo vya malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ni muhimu katika jamii na vitasaidia jamii kuwa na mahali salama kwa malezi ya watoto.

Amesema hatua hiyo ikiungwa mkono na jamii, itasaidia kuunga mkono juhudi jitihada za Serikali kuchochea uchumi wa viwanda ulioiwezesha kufikia Uchumi wa kati.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chamwino, Peter Simba amesema kituo cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kijijini hapo ni neema ya pekee kwao kama kijiji na hivyo watahakikisha wanashirikiana na wadau kuharakisha ujenzi wa kituo hicho ili kitoe huduma inayokusudiwa.

Kwa Upande wake, Ofisa Mradi kutoka Shirika la Brac, Pius Ulaya, amesema Shirika linaunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wake kupitia ujenzi wa vituo hivyo katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam ili kusaidia jamii kuondokana na kero ya watoto kukosa sehemu sahihi za kujifunza na kupata malezi pale wazazi wanapokuwa katika shughuli za maendeleo.

Habari Kubwa