Viwanda, kilimo vilivyoipaisha Tanzania

23Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe
Viwanda, kilimo vilivyoipaisha Tanzania

SEKTA za ujenzi, kilimo na viwanda zimechangia Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kutokana na kuongezeka kwa mchango wake kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019.

Aidha, sekta nyingine ni usafirishaji na uhifadhi mizigo na biashara, ambazo ziliwezesha kuimarika kwa uchumi kwa kuongeza kipato cha wananchi.
 
Akiwasilisha mada ya mapito ya hali ya uchumi nchini katika semina ya waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha, Meneja Msaidizi wa Uchumi na Takwimu wa Banki Kuu ya Tanzania (BoT), Aristeded Mrema, alisema sekta hizo zinagusa maisha ya mwananchi mmoja mmoja.
 
Alizitaja sekta hizo na asilimia zake kwenye mabano ni ujenzi (25), kilimo (20), viwanda (9.6), usafirishaji na uhifadhi mizigo (8.3) na bishara (7.3).
 
Kuhusu mwenendo wa uchumi, alisema unaonyesha kuwa wastani wa kipato kwa kila Mtanzania uliongezeka hadi kufikia wastani wa Dola za Marekani 1,080 mwaka 2019, ikilinganishwa na Dola za Marekani 980, mwaka 2015.
 
Aidha, kuna kuongezeka kwa kipato ambako kumepunguza idadi ya watu walio maskini nchini, kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2017/18.
 
“Uchumi umeendelea kuwa imara katika kipindi cha robo tatu za mwanzo za mwaka 2020 licha ya athari za janga la corona lililoikumba dunia,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Mrema, pato la taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 4.7 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2020, ikilinganishwa na asilimia 7.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2019 na asilimia 6.9 mwaka 2018.
 
“Ukuaji huu umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchukuzi na uchumbaji madini. Pia uamuzi wa serikali kutofunga shughuli za kiuchumi kufuatia mlipuko wa corona,” alisema na kuongeza:
 
“Ukuaji huo ulitokana na uwekezaji ambao serikali imeendelea kufanya katika miundombinu, ukichangia na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi na sera madhubuti ya bajeti ya serikali.”
 
Kwa mujibu wa meneja huyo, matarajio ya ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuwa ni asilimia 5.5 mwaka 2020 na asilimia 6 au zaidi mwaka 2021.

 Nyingine ni sera ya fedha yenye kulenga kuongeza ukwasi na kuongezeka kwa wawekezaji katika sekta binafsi.
 
Kuhusu mfumuko wa bei, alisema umeendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 5 kwa mwaka, na kwamba kwa kipindi cha miaka mitano ulikuwa wa wastani wa asilimia 4.2.
  
Kuhusu mikopo ya benki kwa sekta binafsi, alisema iliongezeka na kukua kwa wastani wa asilimia 8.1 mwaka 2019/20, ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2018/19.

Habari Kubwa