Vodacom yajidhatiti kimafanikio utoaji gawio mwaka wa fedha

18Oct 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Vodacom yajidhatiti kimafanikio utoaji gawio mwaka wa fedha

​​​​​​​KAMPUNI ya Vodacom imesema itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inapata faida na kutoa gawio kwa wanahisa katika mwaka huu wa fedha ikiwa ni baada ya kupata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 30 mwaka uliopita jambo lililosababisha kushindwa kutoa gawio kwa wanahisa wake.

Akizungumza katika mkutano wa wanahisa uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom Jaji mstaafu Thomas Mihayo, amesema hasara hiyo ilisababishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo UVIKO-19.

Jaji Mihayo amesema kutoa gawio kwa kampuni ambazo zimeorodheshwa katika soko la hisa kwao ni kipaumbele, lakini moja ya vitu vilivyoikwamisha kampuni hiyo ni utaratibu wa kusajili laini kwa alama za vidole ambao ulipunguza wateja wa Vodacom zaidi ya milioni 2 na kusababisha kupata hasara kwa zaidi ya asilimia 5.7.

Amebainisha kuwa katika uwasilishaji, mapato ya huduma yaliyoripotiwa ni Sh bilioni 966 ikiwa ni chini ya asilimia 5.7 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Viashiria vingine vilivyoripotiwa ni Sh bilioni 356.8 katika mapato ya M-Pesa na Sh bilioni 186.9 katika mapato ya data, yaliyoongezeka kwa asilimia 3.3.

“Tutafanya kila linalowezekana chini ya sheria ili mwaka huu wanahisa wapate gawio, hatuwezi kusema lazima kwa kuwa hatujui ya mbeleni lakini tumeanza kuona ishara ya matumaini. Mtu kama alikuwa anatumia mashine mbili za kupumulia moja ikiondolewa unashukuru.

“Hakuna kampuni isiyopenda kutoa gawio, uamuzi wa kutotoa gawio ni jambo zito ambalo linamuuma kila mtu ukifikiwa watu hawalali kwakuwa ni kinyime na matarajio ya wanahisa lakini wameridhia katika mkutano mkuu kwakuwa imefanyika hivyo ili kampuni iendelee kustawi,” amesema Jaji Mihayo.

Ameongeza kuwa wanahisa wameafiki agenda zote za mkutano mkuu ikiwemo ya kumwajiri Mkurugenzi Mtendaji Mpya, kuwaongezea muda baadhi ya watendaji na wamekubaliana kuwa ifikapo mwezi Novemba mwaka huu wataangalia mwenendo wa biashara ya kampuni hiyo na taarifa itatolewa kwa wanahisa kwamba wanakwendaje.

Aidha kuhusu tozo mpya zilizoanzishwa na serikali katika mwaka huu wa fedha ni mojawapo ya sababu nyingine iliyotikisa biashara, kwani watu wengi wamepunguza kutuma fedha kwa njia ya mtandao na badala yake wanatumia njia mbadala.

“Kusema kweli tozo zimeathiri biashara baadhi ya watu wameacha kutuma fedha kwa njia ya mtandao nikiwemo mimi mwenyewe ila tunashukuru baada ya serikali kuingilia kati na kupunguza kama asilimia 30 lakini tunaangalia mahesabu bado haijaleta utofauti mkubwa.

“Tunaishukuru serikali kwa kuona kuwa bado iko tayari kutusikiliza kwani imetuambia tuendelee kupeleka maoni yatakayosaidia kuona ni namna gani bora ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo,” amesema Jaji Mihayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ambaye anamaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu, Hisham Hendi ameushukuru uongozi pamoja na wadau mbalimbali wa kampuni hiyo alioshirikiana nao katika kipindi chake chote huku akiwatakia utendaji kazi mwema.

Habari Kubwa