Vyakula, bidhaa zapaisha mfumuko be

11Dec 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Vyakula, bidhaa zapaisha mfumuko be

BIDHAA za vyakula na zisizo za vyakula vimetajwa kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwezi unaoishia Novemba 2019 kwa asilimia 3.8.

Bidhaa hizo ni mchele, nyama, unga wa muhogo, mihogo, mafuta ya kupikia, mboga, maharage, mavazi, mkaa, samani, mazulia na huduma ya malazi ya nyumba za wageni.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja, alipokuwa akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Novemba 2019.

Alisema bei zinaongezeka kutokana na mahitaji ya bidhaa hizo sokoni kuwa makubwa.

"Mahitaji ndio yamesababisha kupanda kwa bei za bidhaa hizi na inawezekana inachangiwa na uhaba wa uzalishaji na usafirishaji," alisema Minja.

Alieleza kuwa mfumuko huo umeongezeka kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019 na kufikia asilimia 3.8 mwaka unaoishia Novemba 2019.

“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba 2019, imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwapo kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019,” alisema.

Alibainisha baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa Novemba 2019 zikilinganishwa na mwezi Novemba 2018, ni pamoja na mchele kwa asilimia 6.6, unga wa muhogo kwa asilimia 7.8, nyama kwa asilimia 2.6, mafuta ya kupikia kwa asilimia 7.2.
Zingine ni maharage kwa asilimia 8.6, mboga kwa asilimia 6 na mihogo kwa asilimia 5.8.

Kadhalika, alisema kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.7, mkaa kwa asilimia 4.4, samani kwa asilimia 3.1, huduma ya malazi kwenye nyumba za wageni kwa asilimia 5 na mazulia kwa asilimia 6.3.

“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Novemba 2019, umeongezeka hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 5.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba 2019,”alisema.

Kuhusu mfumuko kwa nchi zingine, Mkurugenzi huyo alisema nchini Kenya mfumuko umeongezeka hadi asilimia 5.56 kutoka asilimia 4.95 kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019.

“Kwa upande wake Uganda mfumuko umeongezeka hadi asilimia 3 kutoka asilimia 2.5 kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019,” alisema.

Habari Kubwa