Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Emmy Hudson, alisema RITA imepanga kutekeleza hilo kutokana maboresho makubwa katika mfumo wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu hususani katika usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto kupitia mpango wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Alisema mpango huo umeanza na unatekelezwa katika mikoa 18 nchini na kwamba mpaka 2022 utekelezaji katika mikoa nane iliyobaki utakuwa umekamilika.
“Mpango wa usajili wa watoto umesaidia kugatua majukumu ya usajili na kusogeza huduma hiyo karibu na makazi ya wananchi, ambapo huduma za usajili kwa sasa zinatolewa bila malipo, katika vituo vya Tiba na Ofisi za Watendaji Kata,” alisema Hudson.
“Maeneo hayo ni ya kimkakati kwa sababu ni rahisi kwa kila mwananchi kufika na kupatiwa huduma husika. Mtoto anayezaliwa katika kituo cha Tiba anaweza kupata cheti cha kuzaliwa kabla ya kutoka hospitali, cha msingi ni kwa wazazi wenyewe kuandaa jina la mtoto litakalojazwa katika cheti.”
Alisema asilimia 13 ya watoto chini ya miaka mitano waliokuwa wamesajiliwa mwaka 2012 walikuwa asilimia 13 tu na kwamba idadi hiyo imeongezeka na kufikia asilimia 49.4 mwaka 2020.