Vyuo visivyolipa Bima ya Afya vyapewa siku 7

10Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Vyuo visivyolipa Bima ya Afya vyapewa siku 7

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa siku saba kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukutana na wakuu wa vyuo vikuu ili kubaini vyuo ambavyo havijawalipia Bima ya Afya wanafunzi licha ya kulipa ada.

Hatua hiyo imetokana na malalamiko yaliyotolewa na Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), ya kuwapo kwa ucheleweshaji wa vitambulisho vya Bima unaotokana na vyuo kuchelewa kufikisha fedha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa jumuiya hiyo jijini hapa, Majaliwa alimwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kukutana na wakuu hao ili kubaini waliochelewesha fedha hizo na ni kwa wanafunzi wangapi na hatua zipi zimechukuliwa kwa wahusika.

"Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kashughulikie hili kujua wangapi wamelipa ada, wangapi wamepata vitambulisho vya bima na wangapi hawajapata, tatizo ni nini na nani amesababisha, mshughulikiane huko huko, wiki moja inakutosha Katibu Mkuu, hadi Agosti 16, mwaka huu nitakuwa Dodoma nipate taarifa na sababu ya aliyesababisha hilo na hatua zilizochukuliwa," alisema.

Aliwataka wakuu hao kueleza mfumo wanaotumia, kigezo, wangapi wamelipa ada na sababu ya wengine kutopata vitambulisho.

"Kwasasa hakuna migogoro kwenye mikopo na Bodi imetengemaa, hakuna mahali panapochelewa sasa mnataka kuchokoza tena kwenye Bima, nataka nipate taarifa hizi kabla sijaingia kwenye kampeni zangu Ruangwa, na kwa kuwa nitakuwa hapa Dodoma, Mwenyekiti wa TAHLISO kupitia Waziri wa Afya wa vyuo mkaandae taarifa ya malalamiko yote ya waliolipa fedha, lakini hawajapata vitambulisho vya bima ili serikali kuwashughulikia huko vyuo vikuu," alisema.

"Kuna wakati tunakasirisha makundi haya kwa sababu ya mtu mmoja, hatuwezi kukubaliana na hili," alisema.

Alisema hadi sasa Sh. trilioni 4.3 za mikopo ya elimu ya juu zimetolewa tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), na kuwataka waliokopa kurejesha kwa wakati ili kuwanufaisha wengi zaidi.

Alisema fedha hizo zimenufaisha wanafunzi 527,000, hivyo wanufaika hao wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo ili kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.

Awali, Mwenyekiti wa TAHLISO, Peter Niboye, alisema wanajivunia kufanya kazi kwa karibu na Bodi ya Mikopo na Mfuko wa Bima ya Afya na imechangia kutokuwapo na migomo ya wanafunzi.

Aliomba kuwapo na uwakilishi wa Jumuiya hiyo kwenye taasisi muhimu za masuala ya wanafunzi ili kurahisisha kero zao kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

"Pia, kumekuwa na ucheleweshaji wa Bima za Afya tunakuomba Waziri Mkuu fedha hizi wanafunzi walipe moja kwa moja NHIF, kwa kuwa vyuo vimekuwa vikichelewa kuwasilisha fedha hizo na hivyo wanafunzi kuchelewa kupata bima," alisema.

Kuhusu uchaguzi mkuu, alisema jumuiya hiyo inamuunga mkono mlezi wao ambaye ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, katika uchaguzi huo na watahakikisha anashinda kwa kishindo ili kufikia malengo ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.

Habari Kubwa