Vyuo vyapewa saa 48 kulipa wanafunzi

04Jun 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Vyuo vyapewa saa 48 kulipa wanafunzi

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ametoa saa 48 kwa vyuo vikuu nchini kuhakikisha wanafunzi wote wamepewa fedha zao za kujikimu.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, picha mtandao

Amesema chuo chochote ambacho kitakuwa hakijatekeleza agizo hilo hakitakuwa na msamaha zaidi ya kukichukulia hatua.

Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi magari manne yenye thamani ya Sh. milioni 700 kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), yaliyonunuliwa na serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia (WB) uliotolewa kwa ajili ya uboreshaji wa sekta ya elimu nchini.

"Ifikapo Ijumaa wanafunzi wote wa vyuo vikuu wawe wameshapata fedha zao zote za kujikimu, kwa sababu serikali imeshatoa Sh. bilioni 122 kwa ajili yao sasa kwa nini wacheleweshewe? Hakutakuwa na msamaha kwa vyuo ambavyo vitakuwa havijatekeleza agizo hilo," alisema Prof. Ndalichako na kuongeza:

"Rais Magufuli alishatoa maelekezo na lazima yatekelezwe. Sasa ole wao vyuo vitakavyokuwa havijatekeleza agizo hilo, kama kutakuwa na wanafunzi ambao watakuwa hawajasaini fedha za kujikumu achaneni nao wapeni ambao wameshasaini.”

Prof. Ndalichako alisema ni uamuzi unaolenga kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni kwa kuvitaka vyuo vikuu kukamilisha mchakato huo haraka kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kusoma bila changamoto wakati huu ambao wanakabiliwa na ufinyu wa muda kutokana na ratiba ya masomo kusimama kutokana na ugonjwa wa corona.

“Najua wanafunzi wengi kwa sasa wamesharejea vyuoni kuendelea na masomo yao na kama alivyoagiza Rais Magufuli fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi hawa wanapaswa kupewa haraka, nami kwa nafasi hiyo naviagiza vyuo vyote kuhakikisha hadi Ijumaa wanafunzi wawe wamepewa fedha zao, chuo kitakachoshindwa kutekeleza hilo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watakaohusika,” alisema Prof. Ndalichako.

Alisema ni muhimu kwa agizo hilo kutekelezwa kwa wakati bila ya kuwapo kwa visingizio kutoka katika vyuo hivyo kwa kuwa tayari wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ilishajihakikishia kuwa mipango ya utoaji wa fedha hizo upo tayari na kwamba kilichokuwa kikisubiriwa ni mchakato wa vyuo hivyo pamoja na wanafunzi kurejea vyuoni.

“Sitopenda kusikia sababu yoyote hata kama ikionekana kuna mwanafunzi anazembea mwenyewe kujisajili mnaachana naye na kuendelea na wengine, nalisisitiza hili ili kuwakumbusha wahusika wote mtekeleze wajibu wenu ipasavyo," alisema.

Aidha, Prof. Ndalichako aliipongeza NIT kwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo suala inalokisaidia kwenda na mipango mikakati ya serikali ya kuzalisha wataalamu mbalimbali katika sekta ya anga na usafirishaji, hivyo kutoa fursa ya nguvu kazi katika miradi mbalimbali ya serikali.

Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Zacharia Mganilwa, alisema kiasi cha Sh. bilioni 175 kimetolewa na WB kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu nchini, NIT imepata Dola milioni 21.

"Fedha hizi zitatumika kukijengea uwezo chuo, ujenzi wa miundombinu, madarasa, karakana, mabweni na ofisi, vifaa vya kisasa vya kufundishia, pamoja na ununuzi wa ndege tatu za mafunzo," alisema Prof. Mganilwa.

Alisema kutolewa kwa magari hayo kutazidi kuongeza ufanisi kwa chuo hicho ambacho kwa miaka ya hivi karibuni kimeendelea kupiga hatua kubwa za utoaji wa elimu ikiwamo uanzishwaji wa baadhi ya kozi ambazo hapo awali hazikuwapo.

Mbali na NIT, vyuo vingine vitakavyonufaika na fedha hizo ni pamoja na Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA).

Habari Kubwa