Waagizaji magari waomba serikali kupunguza ushuru

19Apr 2022
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waagizaji magari waomba serikali kupunguza ushuru

SIKU chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutamka kuwa magari yaliyotengenezwa chini ya mwaka 2010 yasiingizwe nchini, waagizaji na wauzaji wa magari wameomba serikali ipunguze ushuru ili Watanzania waweze kuyaagiza matoleo mapya.

Aprili 10 mwaka huu, Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kusema Tanzania haitakiwi kuwa dampo kwa kuleta magari yaliyopitwa na wakati.

Wakizungumza na Nipashe  kwa nyakati tofauti, waagizaji na wauzaji wa magari wamesema wateja wao wamekuwa wakiagiza matoleo ya zamani kwa sababu ya bei zake kuwa chini ikilinganishwa na matoleo mapya.

Issa Kinga kutoka Kampuni ya Jan International Limited inayojishughulisha na uuzaji magari, alisema asilimia kubwa ya wateja hununua magari ya mwaka 2005, 2006 na 2008 kutokana na bei yake kuwa chini.

Alitolea mfano kwa wanunuzi wa magari madogo yaliyotengenezwa mwaka 2010 kushuka chini bei zake huwa ndogo ambazo huanzia Sh. milioni 15 kulingana na aina ya gari.

“Alichokisema Waziri Mkuu ni jambo zuri na litatusaidia kuendelea kuwa na magari ya matoleo la kisasa, ila kama wanataka kufanya hivyo washushe ushuru kwa sababu kila Mtanzania ana uwezo wa kununua gari tatizo kubwa huwa ni ushuru mkubwa kuliko bei ya uagizaji gari,” alisema.

Meneja wa SBT Japan ofisi ya Tanzania, Hassan Iddi, alisema mteja anapokwenda kwao na kuchagua gari la toleo la zamani siyo kwamba analipenda zaidi bali ni kutokana na thamani yake sokoni.

“Mfano mtu anataka kuagiza RAV4 ya mwaka 2012 thamani ya kununua gari hilo  Japan ni kubwa na ushuru kwa makisio mteja anatakiwa awe na fedha siyo chini ya milioni 40.

“Wakati RAV 4 toleo la zamani mfano ya 2004 unaweza kutumia Sh. milioni 25 wakati toleo la sasa kuagiza peke yake unaweza kutumia siyo chini ya milioni 20.”

Iddi alisema wateja wengi wa Tanzania kutokana na biashara zilivyo kipato chao hakikidhi magari ya toleo la sasa.

“Siyo kwa watumishi wala wafanyabiashara kwenye asilimia 100 labda wanaoagiza magari ya toleo la sasa ni asilimia tano. Endapo itakuwa hivyo kama walivyoelekeza kwa sababu bado kauli yake haijatolewa ufafanuzi kama yazuiwe kabisa ya chini ya mwaka 2010 au ni mkakati upi utawekwa.

“Labda ya zamani wataongeza kodi kidogo au kuzuia kabisa, wakizuia kabisa maana yake ni kwamba biashara lazima ishuke sana kwa sababu ni kundi dogo la wanaoagiza magari ya sasa.”

Idd alisema  wanasubiri ufafanuzi wa kauli hiyo ili kuelimisha wateja wao kwa sababu tangu itoke wateja walioagiza magari ya chini ya mwaka 2010 wamekuwa wakipiga simu kwao kuulizia hilo.

Kuhusu ushauri wao kwa serikali, Idd alisema wataheshimu maagizo yote yatakayotolewa, ingawa waagizaji wanaona Watanzania wengi kipato chao kinamudu kununua magari ya zamani.

“Sera ingetakiwa iangalie kwa namna gani magari yatakaguliwa hata kama ni ya zamani, kwa sababu hii imeenda sambamba na kubadilisha ukaguzi wa magari kutoka Tanzania na kurudi nje ya nchi, waweke vigezo ya kuangalia ubora wa gari hata kama litaagizwa la 2004 basi liwe katika hali nzuri,” aliomba.

Katika ziara hiyo, Majaliwa alisema Bunge limeshapitisha sheria kuwa magari yote yanayoingizwa nchini yawe yametengenezwa baada ya mwaka 2010 kuja huku mbele.

“Tunaangalia viwango, ni viwango gani wakati sisi siyo watengenezaji, TBS imeeleza maeneo ambayo wanayahakiki magari yetu mengi yanayoingia nchini ni pamoja na yale yanayoagizwa na Watanzania, kama ni kutumika yanakuwa yametumika mwaka mmoja au miwili.

“Sasa yanapokuja hapa lazima tujiridhishe hatuleti magari yaliyopitwa na wakati na Tanzania ikawa dampo, wajibu wa TBS ni kufuatilia gari limetengenezwa lini, je, tairi zilizoingia ni nzima gari lina hali gani, magari mengine mmeyaona ni makukuu.”

Habari Kubwa