Waandishi wa habari wapewa elimu ya chanjo

06Sep 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe Jumapili
Waandishi wa habari wapewa elimu ya chanjo

Waandishi wa Habari kutoka Mkoa wa Mwanza, Mara,Shinyanga na Simiyu wamepewa elimu kuhusiana na huduma za chanjo ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa jamii itakayosaidia kuondoa upotoshaji na kujenga Taifa lenye afya bora.

Akizungumza na waandishi hao jana,  Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk.Dafrosa Lyimo alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa taarifa sahihi kwa wanahabari kuhusiana na huduma za chanjo nchini ili waweze kuandika habari za afya na kufanya tafiti ili kuondoa taarifa zisozosahihi ambazo zitasababisha wananchi kuacha kutumia huduma hizo ambazo Serikali inazitoa .

Alisema katika kipindi hiki wanahabari wanapaswa kuwa mabalozi wa huduma za chanjo, kwa kutumia kila fursa inapopatikana kusaidia kuelimisha jamii umuhimu wa chanjo zote hususani chanjo ya surua, rubella ili kuzui milipuko ya maginjwa hayo.

"Ujumbe muhimu ili mtoto awe na kinga kamili dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo lazima akamilishe chanjo zote kwa wakati kama zilivyo katika ratiba ya chanjo msichana wa umri wa miaka 14 lazima akamilishe dozi mbili za chanjo ya HPV, ikiwa dozi ya pili miezi 6 baada ya kupata dozi ya kwanza pia chanjo zote zinapatikana bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya Serikali, binafsi na mashuleni jamii itambue kuwa chanjo zote ni salama na zimethibitishwa na mamlaka yetu ya dawa na shirika la Afya duniani" alieleza Lyimo. 

Alisema kuwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo yanasambaa kwa kasi kwenye jamii ambayo ina watu wengi ambao hawajapata chajo, hivyo wasiopata chanjo wana nafasi kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya magonjwa kulinganisha na wale waliopata chanjo Jambo la msingi ni kumpatia chanjo mtoto ili kumlinda na kuilinda jamii kwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

"Baadhi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo husababisha ulemavu na vifo, mfano surua husababisha magonjwa ya nimonia, degedege, mtindio wa ubongo, utapiamlo, upofu na vifo ugonjwa wa Rubella husababisha ugonjwa wa moyo kwa watoto, kutokusikia (uziwi), matundu kwenye moyo na madhara ya uti wa mgongo pia polio huleta ulemavu wa viungo na vifo chanjo inabaki kuwa njia rahisi na sahihi ya kumlinda mtoto na kuwa na familia yenye afya." anaeleza Lyimo

Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo ya siku moja kwa wanahabari alisema huduma za chanjo zinazotolewa ni salama na zina manufaa kwa watoto kwani imekuwa msaada kwa kupunguza vifo vya watoto. 

Dk. Subi ameeleza kuwa hadi sasa utoaji chanjo nchini hususan kwa watoto umefikia asilimia 99 kutoka 94 za mwaka 2014, huku uwekezaji katika vifaa tiba na vituo vya kutolea chanjo ukiongezeka, ambapo mwaka 2019/2021 imetengwa bajeti ya Sh Bilioni 30 za chanjo kutoka Sh Bilioni 10 mwaka 2014/15 hivyo wazazi wazingatie huduma ya chanjo ipasavyo ili kuokoa maisha ya watoto wao.

"Kuna baadhi ya magonjwa kama surua, polio na kuharisha yamekomeshwa kutokana na utoaji wa chanjo hizo, ambapo watoto takribani Milioni 2 hadi 3 wameendelea kuokolewa kila mwaka nchini kwa sababu ya utoaji chanjo salama na zilizothibitishwa" alieleza Subi.

Naye Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja akitoa taarifa ya utekelezaji huduma za chanjo na uchanjaji kwa mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka huu, amesema lengo la mkoa huo lilikuwa kuchanja watoto 101,283, na chanjo ya Pepopunda kwa wajawazito 107,968 sambamba na kuwachanja mabinti 27,139 chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi kufatia kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko yazuilikayo kwa njia ya chanjo.

Habari Kubwa