Waandishi Pwani wasaidiwa vifaa vya kujikinga corona

21May 2020
Julieth Mkireri
Kibaha
Nipashe
Waandishi Pwani wasaidiwa vifaa vya kujikinga corona

MDAU wa maendeleo Wilaya ya Kibaha Mjini, Abubakary Alawi, ametoa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 kwa waandishi wa habari mkoani Pwani.

Alawi alisema ametoa msaada huo ili kuwasaidia waandishi kuendelea kujikinga na corona kutokana na mazingira wanayofanyia kazi.

Akikabidhi msaada huo jana katika ofisi za waandishi wa habari mjini Kibaha kwa niaba ya mdau huyo wa maendeleo, Jeremia Komba alisema, utawasaidia waandishi wanapokuwa kazini katika harakati za kuendelea kuuhabarisha umma.

Aliwasihi waandishi kutumia vizuri vifaa hivyo kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu ili waepuke maambukizo ya ugonjwa huo.
Akishukuru baada ya msaada huo, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Pwani (CRPC), Gustaf Haule, alimshukuru mdau huyo kwa kuwakumbuka waandishi.

Haule alisema, msaada huo utawasaidia waandishi wa habari kutokana na kazi ambazo wanakutana na watu mbalimbali katika shughuli zao.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, amesema hali inaendelea vizuri, lakini tunatakiwa tuendelee kujikinga hadi itakapotangazwa kuwa ugonjwa huu umeisha,” alisema Haule.

Pia aliomba wadau wengine kuendelea kujitokeza kusaidia vifaa kinga kwa kundi hilo la waandishi kwa kuwa ni mahitaji yao ya kila siku katika shughuli zao.

Habari Kubwa