Waandishi wa IPP wang’ara wateule tuzo za EJAT 2021

20May 2022
Maulid Mmbaga
DAR
Nipashe
Waandishi wa IPP wang’ara wateule tuzo za EJAT 2021

WAANDISHI 15 wa IPP Media wameng’ara kwa kuwa miongoni mwa wateule 60 wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2021, zinazoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Katika tuzo hizo wateule wa Nipashe ni saba, The Guardian watano na ITV watatu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT, Kajubi Mukajanga, alikusanya jumla ya kazi 598 za kuwania tuzo 20 zilipitiwa na jopo la majaji saba na kupata wateule hao.

Waandishi wa IPP Media walioibuka ni Agusta Njoji, Sanula Athanas, Sabato Kasika, Mary Geofrey, Marco Maduhu, Elizabeth Zaya na Halfani Chusi wa gazeti la  Nipashe.

Kwa upande wa The gazeti la The Guardian ni Muhudini Msamba, Francis Kajubi, Beatrice Philemon, Jenifer Gilla na Christina Mwakangale. Kwa ITV ni Peter Rodgers, Masekepa Masekepa na Jackline Silemu.

Waandishi wa vyombo vingine walioteuliwa na idadi yao kwenye mabano ni Zanzibar Leo (8), Mwananchi (7), Uhuru (1), Habari Leo (1), The Citizen (1), Jamhuri (1), Star TV (4), TBC (1), Azam TV (1), ZBC FM (1), Zanzibar Cable TV (1).

Wengine ni UFM Radio (2), Dar24 online TV (2) na The Chanzo online (2), Shamba FM (1), City FM (1), Highlands FM Radio (1) na CG FM Radio (1), TIFU TV Online (1), Watetezi online TV (1), Nukta.blog (1) na BBC Swahili Online (1).

“Jopo hilo lilitumia siku tisa badala ya nane kutokana na ongezeko la kazi 202 kutoka tuzo za EJAT 2020, ambapo kazi 396 ziliwasilishwa ukilinganisha na kazi 598 za sasa, niwapongeze majaji na kwa kazi kubwa waliyoifanya usiku na mchana ya kupitia kazi hizo,” alisema Mukajanga.

Aliongeza kuwa katika wateule hao, wanawake ni 28 sawa na asilimia 47 ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu, ikilinganishwa na mwaka uliopita walikuwa 26 sawa na asilimia 44.

Aidha, alisema wanaume wateule kwenye tuzo hizo ni 32 sawa na asilimia 53.

Pia, alieleza kuwa kwa mujibu wa majaji, kazi za mwaka huu zimeonyesha kuwa na kiwango cha juu, ikiwamo waandishi wa mtandao kuonyesha kukomaa katika kazi zao na mwamko wa kushiriki tuzo hizo.

Alibainisha kuwa wanatarajia Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika shughuli za utoaji wa tuzo na ndiye atakayemkabidhi tuzo mshindi wa jumla na wa tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari (LAJA) 2022.

Aidha, alifafanua kuwa  tuzo hizo zitatolewa Mei 28, mwaka huu, mkoani  Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya 13 kuwatunza waandishi waliofanya vizuri katika kazi zao za kiuandishi katika mwaka uliopita.

“Baraza linapenda kuwataarifu waandishi wa habari kuwa katika tuzo za mwakani mfumo wa ujazaji fomu utakuwa ni kwa njia ya mtandao (online) ambapo fomu zitajazwa na kutumwa kwa mtandao. Hii itapunguza matumizi ya karatasi na changamoto za CD kukwama kucheza wakati majaji wanapitia kazi,” alisema Mukajanga.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Mkumbwa Ally, alibainisha changamoto mbalimbali walizokutana nazo wakati wanapitia kazi za waandishi, ikiwemo baadhi ya CD kukwama na kutosoma vizuri, hivyo kusababisha shida katika kusikiliza ili kupata kile wanachokihitaji.

Nyingine ni baadhi ya waandishi walifanya makosa katika ujazaji wa fomu hali iliyosababisha wao kushindwa kujua kazi imefanyika kutoka chombo gani na imefanywa na nani huku kazi moja ikifanana na iliyotoka vyombo viwili tofauti.

“Stori nyingi zilikosa namna ya uwasilishaji kuanzia mwanzo wa stori hadi katikati majaji bado walikuwa hawajui mwandishi amelenga nini na baadhi ya waandishi walikuwa hawazingatii vigezo vya kiuandishi kama kupeleka kazi iliyokwisha shiriki miaka iliyopita na kutohoa kazi za waandishi wengine,” alisema Ally.

Habari Kubwa