Waandishi watano wa Azam media wafariki ajalini

08Jul 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Waandishi watano wa Azam media wafariki ajalini

WATU saba wamefariki dunia wakiwamo wafanyakazi wa watano wa Azam TV, katika ajali ya iliyohusisha gari walilokuwa wakisafiria kutokea jijini Dar es Salaam kuelekea wilayani Chato mkoani Geita.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Peter Kakamba, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea saa 2:00 leo katika eneo la Shelui mkoani humo.

Amesema maiti hizo saba miongoni mwao wapo wafanyakazi wa Azam na wengine ambao bado hawajatambulika majina yao.

"Nipo eneo la tukio ni kweli watu saba wamefariki dunia, wakiwamo wafanyakazi wa Azam TV bado tunaendea na uchunguzi wa kutambua majina yao na majeruhi watatu wamekimbizwa hospitali kwa sababu hali zao ni mbaya sana," amesema Kamanda Kakamba.

Aidha, amesema majeruhi watatu wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Igunga mkoani Tabora.

Kuhusu chanzo cha ajali hiyo, amesema wanaendelea na uchunguzi kabla ya kutoa taarifa kamili.