Waathirika wa viboko kulipwa kifuta jasho

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waathirika wa viboko kulipwa kifuta jasho

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, ametoa wiki mbili kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA),-

ishughulikie ombi la wanakijiji cha Chunguruma katika Wilaya ya Mafia mkoani Kibaha, la kulipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi walioathiriwa na wanyama wakali na waharibifu aina ya viboko.

Hatua hiyo inakuja baada ya viboko kuharibu mazao, mifugo pamoja kusababisha kifo cha mwenyekiti wa kijiji hicho, Abdulahaman Musa, mwaka jana.

Viboko wanadaiwa kuharibu mazao, mifugo pamoja na kutishia maisha ya wanakijiji hao na kwamba wamekuwa wakiingia katika nyumba zao nyakati za usiku.

Akizungumza na wanakijiji hao baada ya kusikiliza kilio chao, Kanyasu, alisema tatizo hilo ni kubwa wakati wizara ikitafuta suluhisho la kudumu, itamhamishia askari wanyamapori katika eneo hilo ili waweze kutoa msaada.

"Niwahakikishie tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha maisha yenu yanakuwa salama na hata pale itakapotulazimu tutawapunguza baadhi ya boko ambao wataonekana wanasumbua zaidi,” alisisitiza Kanyasu.

Aliwaeleza kuwa atatuma wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), kujua idadi ya viboko hao kwa kuwa hakuna anayejua idadi yao.

Naye Nassoro Ali ambaye ni mwanakijiji alisema wanyamapori hao ni kivutio cha utalii, lakini wamekuwa kero kwao kwa kuharibu mazao hali inayowasababishia umaskini.

Naye Diwani wa Chunguruma, Hussein Abdi, amemweleza Kanyasu kuwa serikali ifanye haraka kuwalipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa vile ni kilio chao cha muda mrefu.