Waathirika wadai chakula Iringa

27Feb 2016
George Tarimo
Iringa
Nipashe
Waathirika wadai chakula Iringa

Waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Mapogoro, tarafa ya Idodi, wameiomba uongozi wa wilaya ya Iringa kufikisha chakula cha msaada walichopewa kwa lengo la kukabiliana na athari za mafuriko hayo yaliyoacha kaya zaidi ya 70 za kitongoji hicho bila makazi.

Mbunge wa Jimbo la Isimani, Wiliam Lukuvi.

Wakizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Isimani, Wiliam Lukuvi, wananchi hao walisema wanaishi bila ya chakula kwenye kambi ya muda iliyopo katika kijiji cha Mapogoro.

Petro Mbiki ambaye ni mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo alisema kutokufikishwa kwa chakula kwenye kambi hizo za muda kunazidi kuwaathiri kisaikolojia.

Waathirika hao wamepoteza mazao mashambani na nyumba walizokuwa wakiishi na hivyo kutokuwa na uhakika wa maisha ya baadaye.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kijiji cha Mapogoro, Faustine Lova, alisema kuwa baadhi ya waathirika wa mafuriko hayo ambao walipoteza kila kitu kwenye janga hilo walishapewa chakula hicho cha msaada.

Aidha, alisema kijiji kinaendelea kufanya mchakato wa kuendelea kufikisha chakula hicho cha msaada kwa waathirika wote.

Kwa upande wake, Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi alitoa msaada wa Sh. milioni mbili kwa ajili ya kuwalipa fidia watu walio na mashamba kwenye eneo walilohifadhiwa waathirika hao.

Aidha, Lukuvi alitoa Sh. milioni nne kwa ajili ya kurejesha mabomba ya maji yaliyokatika kutokana na kusombwa na mafuriko hayo na kusababisha baadhi ya vijiji vya Mahuninga, Tungamalenga, Kisiriwa na Makifu vilivyopo kwenye tarafa hiyo kukosa maji safi na salama ya kunywa.

Mafuriko hayo katika kijiji cha Mapogoro yalitokea Januari 29 baada ya Mto Mapogoro kukata kingo na kuacha njia yake.

Habari Kubwa