Wabunge Chadema watangaza kuhamia NCCR-Mageuzi

23May 2020
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Wabunge Chadema watangaza kuhamia NCCR-Mageuzi

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wametangaza kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi baada ya Bunge la 11 kuvunjwa huku wakikituhumu chama hicho kwa kuvunja misingi ya Katiba.

Wabunge hao waliotangaza kukihama chama hicho ni Joyce Sokombi na Susanne Maselle wa Viti Maalum.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, walisema wamehama Chadema kutokana na kutoheshimika kwa Katiba ilhali ndio msingi mkuu wa kuanzishwa kwa mageuzi nchini.

Madai mengine ni kukiukwa kwa haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa na kutoa mfano kwa wabunge wanne walioondolewa wakiwamo Wilfred Lwakatare, Joseph Selasini, Anthony Komu na David Silinde, ambao wote walifukuzwa uanachama bila kusikilizwa.

“Natural Justice (usawa wa haki) iko wapi hapo wakati haki hiyo ipo ndani ya katiba ya chama hiki ambacho leo hii wabunge wake wanafukuzwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa,” walihoji.

Kadhalika, walisema sababu nyingine ni kukiukwa haki ya kuhoji matumizi ya michango na fedha za ruzuku na kutoa mfano kwa wabunge wa viti maalumu kila mmoja kwa mwezi walikuwa wanachangia chama Sh. 1,550,000 tangu Januari 2016 mpaka Aprili 2019, ambazo matumizi yake hayafahamiki.

“Ndani ya miezi 40 kila mmoja wetu amechangia chama takriban Sh. milioni 62, wabunge wa viti maalum tupo 37, hivyo tumechangia zaidi ya Sh. bilioni 2.2, hoja yetu hatulalamiki kuchangia hapa chama bali ni wajibu wetu kuhoji fedha hizi matumizi yake hayajawahi kuwekwa wazi na haturuhusiwi kuhoji popote.”

Walidai kuwa chama kimekuwa kikihodhiwa madaraka yake kwa wabunge wachache na wengi wao ni wanaume na hivyo kuwapo kwa mwanya wa unyanyasaji wa kijinsia na kingono.

Wabunge hao walidai hoja zingine ni kuwapo ndani ya chama hicho mgawanyiko mkubwa unaotokana na baadhi ya watu kujiona wao ni bora kuliko wengine na jitihada za kutaka kuondokana na hali hiyo kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu zimeshindikana.

Vile vile, walidai kuwa ndani ya chama hicho kuna makundi ya kibaguzi hadi bungeni na kutaja upande wabunge wa viti maalum uchangiaji katika vikao vya bunge unaenda kwa kufahamiana na wengine kufanywa wapiga makofi na kuitwa wabunge maarufu (Super Star).

Walidai sababu zingine zilizowavutia kuhamia NCCR- Mageuzi ni mfumo wa kuendesha chama kitaasisi, na itikadi yake ya utu ambao msingi wake mkuu ni haki za binadamu.

Pia, walisema katiba yake imewekwa wazi usawa wa jinsia kwa viongozi wakuu wa juu kama Makamu Mwenyekiti wa Taifa na Katibu Mkuu ni wanawake huku katiba na kanuni za uendeshaji wa chama zimeziba mianya ya uvunjifu wa amani ndani ya chama na nje kwa maslahi ya kulinda amani ya nchi.

Walisema chama kimekuwa na utulivu wa kisiasa kwa kuweka maslahi ya taifa mbele kabla ya mengine, ikiwa ni kujikita kwenye kuboresha elimu kwa Watanzania kwa hoja na vitendo.

Habari Kubwa