Wabunge mtegoni kukacha kikao CCM

22Feb 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wabunge mtegoni kukacha kikao CCM

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Donald Magesa, ameagiza wabunge wote wa CCM mkoani hapa kuandika barua kujieleza kwa nini hawajahudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.

Magesa alisema hayo jana kwenye kikao hiocho kilichokuwa na lengo la kusoma taarifa ya utekelezaji ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuanzisha Januari, 2016 hadi Desemba, mwaka jana.

Alisema haiwezekani baadhi ya wabunge wa mkoa huo wasiwapo kwenye kikao hicho bila ya kutoa taarifa yoyote wakati wao ni wajumbe muhimu wa utekelezaji wa ilani hiyo.

"Naagiza makatibu wa wilaya wa CCM, mkalisimamie hili wabunge wote ambao hawajahudhuria kikao hiki, waandike barua za maelezo," alisema Magesa.

"Na bahati nzuri mimi ndio msimamizi wa uchaguzi ngazi ya chama na wasipohudhuria kikao kingine nitajua nini cha kufanya. Wasifanye chama kuwa lifti ya mafanikio yao," aliongeza.

Wabunge waliohudhuria kikao hicho ni Eliai Kwandikwa (Ushetu), Ezikiel Maige (Msalala)na Azza Hilal wa Viti Maalum.

Wabunge ambao hawakuhudhulia ni Stephen Masele (Shinyanga Mjini), Ahmed Salum (Solwa), Jumanne Kishimba (Kahama Mjini), Suleiman Nchambi (Kishapu) na Lucy Mayenga (Viti Maalum).

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, alisema imetekelezwa kwa kiwango kikubwa zikiwamo sekta za kilimo, elimu, afya, maji, viwanda, ardhi, madini, nishati na barabara.

Habari Kubwa