Wabunge upinzani wahoji kauli ya Mkuu wa Majeshi

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Wabunge upinzani wahoji kauli ya Mkuu wa Majeshi
  • *Ni inayohusu jeshi kufuatilia wanaotoa kauli za uchochezi 

BAADHI ya wabunge wa upinzani, wamehoji bungeni kauli iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo, kuhusu jeshi kufuatilia wanaotoa kauli zenye lengo la kuvuruga amani ya nchi.

Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema), picha mtandao

Juzi, wakati Rais John Magufuli akizindua mji wa kiserikali Mtumba jijini Dodoma, Jenerali Mabeyo alisema jeshi linafuatilia kauli tata zenye lengo la kuleta uchochezi na kuvuruga amani ya nchi.

Wakichangia makadirio ya wizara mbili zilizoko chini ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utumishi) kwa mwaka ujao wa fedha, baadhi ya wabunge wa upinzani walihoji sababu za Jenerali Mabeyo kutoa kauli hiyo wakidai si jukumu lake.

Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema), alisema Jenerali Mabeyo hakupaswa kutoa kauli hiyo kwa kuwa ufuatiliaji wa wachochezi unafanywa na Jeshi la Polisi, hivyo ilipaswa kutolewa na mkuu wa jeshi hilo.

Mbunge wa Mlimba, Susan Kiwanga (Chadema), alihoji sababu za Mkuu wa Majeshi kuchunguza mambo ya uchochezi wa wanasiasa.

"Tumesikia kwenye vyombo vya habari kuwa Mkuu wa Majeshi anachunguza kauli za uchochezi zinazohatarisha amani. Sasa watu wa utawala bora nataka mnijibu, Mkuu wa Majeshi amekuwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka)? Nakemea kwa nguvu zote na ashindwe kwa jina la Yesu," Kiwanga alisema.

Wakati mbunge huyo akiendelea kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisimama kuomba kutoa taarifa bungeni.

Alipopewa nafasi hiyo, Mhagama ambaye pia ni Mnadhimu wa Serikali Bungeni, alisema Jenerali Mabeyo hakusema anawachunguza wanasiasa.

"Mheshimiwa Naibu Spika, alichozungumzia CDF (Mkuu wa Majeshi) ni masuala ya amani, ulinzi na usalama kwa ujumla. Hakusema wanasiasa, hili lazima tuliweke sawa," Mhagama alisema.

Kutokana na kauli hiyo ya Mhagama, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho cha Bunge, aliwataka wabunge wasitoe kauli ambazo hawana uhakika nazo.

"Tuwe waangalifu. Wakati mwingine tusitoe kauli ambazo hatuna uhakika nazo kwa sababu siku hiyo (Jumamosi) hata mimi nilikuwapo na (Jenerali Mabeyo) alisema wanafuatilia siyo wanachunguza," Dk. Tulia alisema.

Katika mchango wake kuhusu hoja ya makadirio ya bajeti ya wizara hizo mbili, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tamisemi, Mwita Waitara, alisema kama kuna chokochoko zenye kuashiria uvunjifu wa amani zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa, Jenerali Mabeyo hapaswi kukaa kimya.

"Hivi Mkuu wa Majeshi anayeangalia ulinzi wa nchi hii, hautaki atoe kauli dhidi ya wachochezi?" Waitara alihoji. "Haiwezekani mbunge aseme patachimbika, huu mchezo hauhitaji dakika tisini, wao wapo na sisi tupo. Maneno kama hayo ya uchochezi na fujo, serikali haitayavumilia.

"Nashangaa sana hiyo demokrasia inayozungumzwa, wakati Mch. (Peter) Msigwa alipokuwa akigombea uenyekiti wa kanda wa Chadema, wagombea wote waliondolewa na akapata asilimia 48 ya kura ya hapana.

"Tunataka wanasiasa wa upinzani makini kama (Joseph) Selasini au James Mbatia, wamewasilisha hoja zao vizuri na kwenye maeneo yaliyokuwa na changamoto kama wakuu wa mikoa, tumeshazungumza nao na ile ya mfuko wa jimbo imeshatatuliwa.


"Alikuja Prof. Patrice Lumumba, anasema 'Magufulification of Africa', yaani Rais Magufuli ana sifa ya kuwa kiongozi wa Afrika kupitia miradi ya kimkakati anayoitekeleza."

Habari Kubwa