Wabunge, vigogo wa CCM watimuliwa uchaguzi wazazi

06Jan 2019
Elisante John
Singida
Nipashe Jumapili
Wabunge, vigogo wa CCM watimuliwa uchaguzi wazazi

UCHAGUZI mdogo wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti Wazazi Mkoa Singida, ulifanyika jana nchini kwa tahadhari kubwa baada ya msimamizi mkuu kuwatoa ukumbini viongozi waandamizi, akiwemo Mwenyekiti CCM wa Mkoa na wabunge.

Dk. Mwigulu Nchemba

Waliokutana na adha hiyo ni Mwenyekiti Juma Kilimba, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara na Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk. Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka, Mbunge Iramba Mashariki, Allan Kiula na Mbunge Singida Magharibi, Elibariki Kingu.

 

Wengine ni Meya Manispaa Singida, Mbua Chima Gwae, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi, Ali Minja na James Mkwega wa Halmashauri ya Wilaya ya  Mkalama.

 

Ingawa walikuwa na barua za mwaliko kwa ajili ya upigaji kura huku vifuani wakiwa wamevalia nembo zilizoandikwa ‘MJUMBE’, viongozi hao walijikongoja taratibu huku baadhi ya wahudumu wa chama hicho wakiangua vicheko nje ya ukumbi wa chuo cha VETA, ulikofanyika uchaguzi huo.

 

Sakata hilo liliwahusisha pia wanahabari na wanausalama, wakiwamo maofisa wa  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), hivyo kwa ujumla wao wote wakatii amri hiyo na kutoka ukumbini katika hali ya unyonge.

 

Baada ya mkutano huo maalumu wa uchaguzi kufunguliwa na mwenyekiti aliyeachia nafasi hiyo kutokana na kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wazazi Taifa, Erasto Sima, msimamizi wa uchaguzi, Paul Kirigini, alitangaza waalikwa wote watoke nje ya ukumbi.

 

Katika tangazo lake, Kirigini alifafanua kuwa waandishi na waalikwa wengine wapishe, lakini kama vile haitoshi, akaongeza kuwa: “Pia wabunge, wenyeviti wa halmashauri, meya na Mwenyekiti wa CCM Mkoa nao si wajumbe wa mkutano huu wa uchaguzi, tunaomba watoke.”

 

Viongozi hao waandamizi walipotoka ukumbini na kuungana na wanahabari waliokuwa wa kwanza kutoka, walianza kunung’unika kuwa uchaguzi huo una kitu gani cha ziada tofauti na uliopita wowote, zaidi ya kuwadhalilisha ingawa walikuwa na mialiko halali.

 

“Jambo hili si nzuri, hata kama sisi si wajumbe tulipaswa kuwamo ndani ya ukumbi kama waangalizi kwa sababu ni viongozi wakuu wa CCM. Naomba karatasi nimwandikie ujumbe msimamizi wa uchaguzi,” alilalamika Killimbah.

 

Aliungwa mkono na Dk. Nchemba ambaye alishangazwa na hali hiyo na kuwataka wenzake watoke ili kutii agizo.

 

“Hii ndio tatizo la kustaafu ukiwa bado kijana, watu hawakuheshimu. Mimi nimewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, wewe ni Mwenyekiti wa Mkoa na ninyi ni Wabunge… ndio watengeneza sera, sasa leo (jana) tunaamriwa kutoka nje ya ukumbi,” alisema Dk. Nchemba.

 

Wakiendelea kujadiliana nje ya ukumbi, ghafla ikasikika sauti kwa njia ya kipaza sauti kuwa watoke nje ya la lango kuu lililoko zaidi ya mita 200, ambako walikutana na ulinzi mkali wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) ambao waliwafungulia lango na kutoka.

 

Baadaye wakiwa nje ya lango, walianza kuwapigia simu madereva wao ambao tayari walikwisharudi mjini zaidi ya kilomita tano, ili wakawachukue kwa ajili ya safari za kwenda kwenye makazi na shughuli zao.

 

Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi za CCM, waalikwa huwamo ndani ya ukumbi mpaka wagombea wanapojieleza, kisha wakati wa upigaji kura hutakiwa kutoka ukumbini kusubiri muda wa kutangaza matokeo.

 

Awali, akifungua mkutano huo, Sima aliwataka wajumbe na wana- CCM kuendelea kupendana ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kurudisha nyuma jitihada za kujenga chama chao, Killimbah akiwataka watumie vyema haki yao katiba kwa kuchagua kiongozi bora.

 

Katika uchaguzi huo, wanachama wanne wa CCM waliteuliwa kuwania nafasi hiyo akiwemo Mwenyekiti wa Singida United, Yusufu Mwandami aliyewahi pia kushika nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

 

Wengine ni Salum Chima ambaye aliwahi kuwa katibu Tawala wa Mkoa, mtaalamu wa shughuli za ufugaji nyuki, Philemon Kiemi, na mwanamama mchimba madini Bertha Nakoroma.

 

Habari Kubwa