Wabunge wapewa notisi kuhama nuimba za serikali

22May 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Wabunge wapewa notisi kuhama nuimba za serikali

WAKATI Bunge la 11 likitarajiwa kumalizika Juni 19, mwaka huu, imeelezwa kuwa wabunge waliopanga katika nyumba za serikali mjini Dodoma, wameanza kupewa barua za kutakiwa kuondoka.

Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa, aliyasema hayo jana bungeni wakati akiomba mwongozo wa spika kuhusu suala hilo, huku akimwomba Spika Job Ndugai, kuzungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, kuliangalia upya suala hilo na kuwa na subira hadi uchaguzi utakapomalizika.

Mchengerwa alisema asilimia 99 ya wabunge wamepewa barua na Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA), zinazowataka kuondoka haraka katika nyumba za serikali walizokuwa wamepanga.

“Wabunge wengi wameshapewa barua ya kutakiwa kuondoka katika nyumba za serikali na wametakiwa ndani ya muda mfupi wawe wameshaondoka,” alisema Mchengerwa na kuongeza:

“Asilimia 99 ya wabunge waliopewa barua hizo ni wa CCM, nikuombe Spika kwa kutambua kazi kubwa wanayoifanya wabunge. Na kutambua shughuli za kibunge zipo Dodoma na Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi, nikuombe Spika umuombe Waziri wa Ujenzi atusaidie, iwapo serikali wanataka kutekeleza agizo hili wasubiri hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika ndipo wabunge wapatiwe barua hizo,” alisema Mchengerwa.

Mchengerwa alisema wabunge walioingia katika nyumba hizo walizikuta chakavu na nyingine mbovu, hivyo walitumia fedha nyingi kuzikarabati.

Alisema wabunge wengine walitumia Sh. milioni tano hadi 10, hivyo Waziri wa Ujenzi anapaswa kulizingatia suala hilo.

Mchengerwa alisema TBA inapaswa kusubiri hadi uchaguzi mkuu ufanyike, na kwamba kwa wabunge watakaopata nafasi ya kuchaguliwa tena wapewe nafasi ya kuendelea kukaa katika nyumba hizo.

WAZIRI ATOA UFAFANUZI

Waziri Kamwelwe akijibu hoja hiyo alikiri kuwapo kwa utolewaji wa barua kwa wabunge waliopanga nyumba za serikali wakitakiwa kuondoka haraka.

“Wapo wabunge walioingia mikataba na TBA kwa makubalinao kwamba Bunge ndilo litakuwa linawalipia kodi, wabunge wengine waliingia mikataba ya kujilipia wenyewe kodi,” alisema Kamwelwe na kuongeza:

“Kwa sababu suala hili ni la mikataba, Bunge linaisha mwezi wa sita, wabunge wanaolipiwa na bunge mkataba wao utakuwa umeisha, ndiyo maana TBA wameamua kufanya hivyo. Ila wale ambao wanalipa kodi wenyewe wanaweza kujibu barua hiyo,

nikiwamo mimi nimesaini mkataba wa kulipa kodi mwenyewe. Hivyo kama nitapata barua nitawajibu kuwa bado nipo,” alisema Kamwele.

MAELEZO YA SPIKA

Akilitolea ufafanuzi zaidi suala hilo, Spika Job Ndugai, alisema: “Hapa waziri anamaanisha Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi, hivyo wabunge jengeni msipende kupanga. Ila hakutaka kusema tuu, ila ndiyo ujumbe wenyewe.”

“Anayetaka kiwanja amuone Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo, ukikosa kiwanja mfuate Waziri wa Ardhi, Willium Lukuvi. Sisi tulioingia bungeni mwaka 2000 tulipewa viwanja, nikiwamo mimi, juzi nilienda kukifuatilia nikakuta kimechukuliwa, lakini nimekirudisha,” alisema Spika Ndugai.

Spika Ndugai aliwataka wabunge ambao wanauhitaji wa kweli wa viwanja wamuone ili awasaidie.

Alisema: “Wabunge wenzetu wa Uganda hawamalizi ubunge bila ya kuwa na nyumba katika Jiji la Kampala, hata Kenya mbunge hamalizi ubunge bila ya kuwa na nyumba Nairobi.”

Habari Kubwa