Wabunge wataka adhabu kali kwa mafataki

28Jun 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wabunge wataka adhabu kali kwa mafataki

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016, huku wabunge wakitaka adhabu zaidi iongezwe kwa atakayempa ujauzito mwanafunzi na atoe na fedha za matunzo kwa mtoto.

Wakati Wabunge wakipendekeza hivyo, pia serikali imeondoa faini kwa watu waliokuwa wakikutwa na makosa ya kuwapa mimba watoto wenye umri wa miaka 18, hivyo kwa sasa watatumikia kifungo gerezani.

Muswada huo uliowasiliswa Juni 24, mwaka huu, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, pamoja na mambo mengine, kwa upande wa elimu unalenga kuweka masharti yanayojitosheleza kuhusu zuio la kuoa au kumpatia mimba mwanafunzi.

Wakichangia jana mjadala wa muswada huo, wabunge walipongeza marekebisho ya sheria ya elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela kwa mtu yeyote atakayeoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, wakidai adhabu hiyo bado haitoshi.

Pia baadhi ya wabunge walitoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza vinasaba (DNA) kabla ya kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo na viboko.

Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu, alisema ni vyema adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchwapwa viboko 12 kila mwezi.

Subira Mgalu (Viti Maalum- CCM), alisema pamoja na marekebisho hayo, pia waangalie namna ya kukabiliana na utoro kwenye shule ili kuwafanya wanafunzi kupata elimu.

Hata hivyo, Mbunge wa Njombe Kusini (CCM), Edward Mwalongo, alitaka sheria hiyo ielekeze anayekutwa na kosa kuacha fedha za fidia ambazo mama atazitumia wakati mwanamume yuko jela.

Akijibu hoja za wabunge, Masaju alisema kwa sasa utaratibu wa vipimo vya DNA kwa sasa unatumika ili mahakama na waendesha mashtaka kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi kutokana na Tanzania kutokuwa na uwezo wa kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.

Aidha, Masaju aliwataka wazazi nchini kuzingatia malezi ya watoto wao ili kuepusha migongano katika jamii.

Alisema marekebisho ya sheria hizo, serikali imezingatia mahitaji ya sasa, katika kufanyia marekebisho sheria lengo likiwa ni kuondoa upungufu ambao umeathiri wakati wa kutumia sheria hizo kwa kuongeza masharti mbalimbali ili kuleta uwiano kati ya sheria zilizorekebishwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama, kwa upande wake alisema serikali imekuja na sheria hiyo ili kuwabana waajiri wanaochelewesha michango ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza sheria Waziri ataweka makundi na kuwa kampuni zenye kipato kikubwa adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.

Sheria zingine zilizofanyiwa marekebisho ni za kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu sura ya 423, kuzuia usafarishaji wa binadamu sura ya 432, kanuni za madai sura ya 33, usajili wa makandarasi sura ya 235, taasisi za kazi sura ya 300, ushahidi sura ya 6 na misitu sura ya 323.

Zingine ni uhamiaji sura ya 54, ajira na uhusiano kazini sura ya 366, mtoto sura ya 13, mahakama za migogoro ya ardhi sura 216, afya ya akili sura ya 98, Baraza la Kiswahili Tanzania sura ya 52 na viapo sura ya 12.

Pia zimo sheria za kanuni ya adhabu sura ya 16, kuzuia ugaidi sura ya 19, usimamizi wa mirathi sura ya 352, Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283 na maadili ya viongozi wa umma sura ya 398.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa