Wabunge wazidi kumbana Prof. Kabudi

16May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Wabunge wazidi kumbana Prof. Kabudi

BAADHI ya wabunge wameendelea kumtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, kujiuzuu ili kuonyesha kuwajibika kutokana na kile walichokiita ushauri wake mbovu kwa serikali.

Hoja ya kumtaka Prof. Kabudi kujiuzulu ilitolewa juzi bungeni na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iipowasilisha hotuba yake kuhusu makadirio ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka ujao wa fedha.

Kambi hiyo iliwataka Prof. Kabudi, Mawaziri wa Viwanda, Biashara na Wizara ya Kilimo na maofisa wote walioshiriki kutia saini makubaliano ya serikali na Kampuni ya Indo Power ya Kenya kwa ajili ya ununuzi wa korosho, kujiuzulu kutokana na uamuzi wao huo kuisababishia serikali hasara ya Sh. trilioni 1.18.

Akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo jana, Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), aliendeleza hoja hiyo akimtaka Prof. Kabudi kujiuzulu kwa kuwa ameitia hasara serikali.

Komu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, alisema Prof. Kabudi ndiye anapaswa kuwa mtu wa kwanza wa serikali aliyeshuhudia kutiwa saini kwa makubaliano ya serikali na kampuni hiyo ya Kenya, kujiuzulu kwa uamuzi wake umekuwa mara nyingi ukisababisha shida kwa taifa.

Kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

"Prof. Kabudi ndiye tatizo kwa nchi hii, ameliingiza taifa hili kwenye matatizo makubwa. Kwa mfano, kwenye korosho, Sheria ya Takwimu, Mpango wa PPP (Ubia wa pamoja katika ya sekta ya umma na binafsi), makinikia na mingine mingi tu," Komu alisema.

Mbunge huyo alilishauri Bunge kuchukua hatua za kumwajibisha waziri huyo kwa kile alichoeleza kuwa amekuwa akifanya uamuzi mbovu na kuwadanganya Watanzania.

Alisema licha ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana kuwataka Waziri wa Kilimo na Waziri wa Viwanda na Biashara kujiuzulu, yeye anaona waziri wa kujiuzulu kwa sasa ni Prof. Kabudi, akidai wawili hao (Japhet Hasunga na Joseph Kakunda) "wapo ndani ya basi tu, lakini hawajui kinachoendelea."

Hoja hiyo ya kumtaka Prof. Kabudi kuwajibika, pia iliungwa mkono na Mbunge wa Tandahimba, Ahmed Katani (CUF), ambaye alisema kampuni hiyo ya Kenya ililenga kuwatapeli wakulima wa korosho.

Awali akichangia mjadala huo, Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel (CCM), alisema serikali haipaswi kupuuza malalamiko ya wabunge, akieleza kuwa ni vigumu kuwekeza nchini kama gharama ya umeme zitaendelea kuwa juu.

"Kwa kuliona hilo, ndiyo maana Rais Magufuli ameamua kuwekeza katika mradi wa umeme wa Stiegler's Gorge. Nilipokuwa kule (upinzani), nilihama na kauli yangu kuungana na wazalendo, kulinda maslahi ya taifa," alisema.