Wabunifu majengo watakiwa kujitathmini

25Nov 2018
Yasmine Protace
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wabunifu majengo watakiwa kujitathmini

SERIKALI imewataka wakadiriaji ujenzi nchini kuangalia namna ya kupunguza gharama za ujenzi wa majengo ili kutoishitua serikali kwenye shughuli za ujenzi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, picha na mtandao

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema hayo juzi alipokuwa akifungua semina ya kitaalamu ya elimu endelevu kwa wabunifu majengo na wakadiriaji ujenzi iliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) Dar es Salaam.

Alisema serikali inatambua umuhimu wa kuwatumia wabunifu majengo na wakadiriaji ujenzi katika kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma.

Alisema pamoja na baadhi ya taasisi kuendelea kuwatumia watu wasio na utaalamu katika kusimamia miradi ya umma, iko haja kwa watalaam wa fani hizo kujitizama upya na kuangalia wapi wanapokosea ili waaminike katika jamii.

Alisema wamekuwa wakilalamikiwa na jamii kwa kuwa na gharama kubwa tofauti na matarajio ya wengi kwamba kuwatumia wataalamu hao mtu atapata nafuu katika ujenzi.

"Jitizameni upya na mwangalie namna ya kuhakikisha mnaaminika kwa jamii pale mnapofanya makadirio ya ujenzi ili mpate tenda katika miradi mbalimbali ya serikali na kwa watu binafsi pale wanapotaka kujenga nyumba zao," alisisitiza.

Hata hivyo, aliipongeza AQRB kwa jitihada inazofanya katika kuandaa mkakati wa mawasiliano ili iwe njia pekee ya kutangaza shughuli zao huku akiwasisitiza kuacha kukaa ofisini badala yake wazifuate fursa ziliko.

Kaimu Msajili wa AQRB, Albert Munuo, alisema majukumu ya wataalam hao ni pamoja na kuhakikisha waendelezaji wa ujenzi wa majengo na miundombinu wanapatiwa huduma stahiki ili wapate majengo na miundombinu bora yenye gharama stahiki.

Alisema hadi Oktoba 31, mwaka huu, bodi imesajili wataalamu 1,640 na kampuni za kitaalamu 417, ikiwa ni ongezeko la asilimia 872 kwa wataalamu na asilimia 787 kwa kampuni.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Ludigija Bulamile, aliyataja mambo muhimu katika sekta ya ujenzi kuwa ni pamoja na kuwawezesha wadau kutambua namna bora ya kushindana katika soko la pamoja la nchi za Afrika Mashariki.

Zingne ni matumizi bora ya nishati endelevu katika majengo kwa kuwa matumizi bora ya nishati yanatokana na ubunifu bora wa jengo.

Habari Kubwa