Wachambuzi wa siasa watoa sababu ‘mafuriko’

15Jul 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Wachambuzi wa siasa watoa sababu ‘mafuriko’

WACHAMBUZI wa siasa nchini wamesema sababu ya kuwapo kwa mwamko mkubwa wa watu kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania ubunge ni kupanuka kwa uwanja wa kisiasa nchini pamoja na kuhitaji kuteuliwa kushika nafasi za uongozi.

Wakizungumza na Nipashe wachambuzi hao pia wamesema sababu nyingine huenda ni njia mojawapo ya kupata maisha mazuri kirahisi, kukidhi mahitaji yao.

Tangu kufunguliwa kwa dirisha la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali hususani ubunge kwa vyama vya siasa nchini, kumekuwa na 'utitiri' wa wagombea wanaojitokeza katika majimbo mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani.

Hadi jana jioni, Nipashe ilishuhudia idadi kubwa ya wagombea wakijitokeza kuchukua fomu za kuteuliwa kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo moja, huku mteule anayehitajika ni mmoja tu.

Akizungumzia hali hiyo, Dk. Bakari Mohammed kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema ubunge umeonekana kuwa ni ‘dili’ nyakati hizi.

"Wengine wamechukua fomu kwa ajili ya kuhudumia jamii, wengine wamechukua fomu kwa sababu wanataka ajira pamoja na kukidhi mahitaji yao," alisema Dk. Bakari.

Aliongeza kuwa: "Ni njia ya 'short cut' (fupi) ya kujikwamua kiuchumi, wengi wanadhani kwamba wakipata ubunge watakuwa wamejikwamua kimaisha. Lakini mwamko ni mkubwa kisiasa na tutarajie idadi kubwa zaidi."

Naye Dk. Richard Sambaiga, kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, UDSM, alisema kilichobadilika mwaka 2015 na mwaka huu ni muktadha wa kufanya siasa pamoja na kupanuka kwa uwanja wa siasa.

Alisema idadi kubwa ya watia nia waliojitokeza majimboni wanatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya mabadiliko yaliyofanywa na chama hicho.

Dk. Sambaiga alisema miaka ya nyumba ndani ya CCM mgombea ambaye alikuwa hana pesa kushinda kura za maoni ilikuwa ni ngumu.

"Wanadhani uwanja wa kufanya siasa umepanuka, ile dhana kwamba ubunge ni kuwa na pesa imetoweka, Reform (mabadiliko) ndani ya chama ndiyo imewashawishi wanachama," alisema Dk. Sambaiga.

Pia Dk. Sambaiga alisema sababu nyingine ni wagombea kuhitaji nafasi za uteuzi siku zijazo.

"Wanahitaji kukumbukwa mbeleni kwenye uteuzi na hawa ni vijana, wameona kwamba ukipata fursa ya kuwania unaweza kukumbukwa."

Kwa upande wake wakili wa kujitegemea kutoka Mahakama Kuu ya Zanzibar, Othman Masoud, alisema sababu kubwa ni kuongezeka kwa kiwango cha elimu ya uraia.

Sababu nyingine aliitaja ni bunge lililopita lilishawishi watu wengi katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, kutokana na hoja na mijadala iliyokuwa ikijadiliwa.

Alisema: "Hali ya kimaisha nayo imechochea, kote bara na visiwani, hali ya kimaisha ilibana sana hivyo wameamua kukimbilia kwenye ubunge ili kujikidhi kimaisha."

Habari Kubwa