Wachangisha mil. 450/- za kuboresha kituo cha afya

28May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Wachangisha mil. 450/- za kuboresha kituo cha afya

KANISA la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa mkoani Dodoma lina mpango wa kuchangisha zaidi ya Sh. milioni 450 kwa lengo la kutanua na kuboresha kituo chake cha afya cha St. Lukes.

Askofu wa Dayosisi hiyo, Jacob Chimeledya na  Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Tom Mazanda, walisema uamuzi wa kuanzisha mradi huo wa upanuzi ikiwamo kujenga wodi ya wanawake na watoto, upanuzi wa maabara, kununua vifaa vya afya na kuongeza watendaji umetokana na mahitaji yaliyopo katika kituo hicho ambacho kinahudumia watu wengi.

Kamati ya Maandalizi, Tom Mazanda, walisema uamuzi wa kuanzisha mradi huo wa upanuzi ikiwamo kujenga wodi ya wanawake na watoto, upanuzi wa maabara, kununua vifaa vya afya na kuongeza watendaji umetokana na mahitaji yaliyopo katika kituo hicho ambacho kinahudumia watu wengi.
 
“Wana Mpwapwa wanatambua umuhimu wa kituo hiki cha St Lukes na ndio maana tumeamua kuungana na kuangalia namna ya kuchangisha fedha za kuwezesha mradi huo,” walisema kuitia taarifa kwa vyombo vya habari.
 
Mganga Mkuu wa kituo hicho, Dk. Edwin Kiula, alisema kituo kilisajiliwa rasmi mwaka 1993 kama zahanati kutoka kwa Wamishionari wa CMS walioanzisha huduma za afya katika eneo hilo toka mwaka 1876.
 
Kituo cha Afya cha St. Lukes kwa sasa kinahudumia wastani wa wagonjwa kati ya 50 na 60 kwa siku, wanawake wanaojifungua kwa mwaka ni kati ya 550 na 600.
 
Kwa mujibu wa Dk. Kiula, wanawake wanaotibiwa magonjwa mengine ya kinamama ni zaidi ya 400 na watoto wanaolazwa ni wastani wa 300 kwa mwaka, wakati wagonjwa wa nje (OPD) kwa ujumla ni 11,000 hadi 13,000 kwa mwaka kliniki ya wajawazito na watoto ina wastani wa mahudhurio 18,000 hadi 20,000 kwa mwaka.
 
Magonjwa yanayotibiwa sana katika kituo hicho ni maradhi ya via vya uzazi (PID), nimonia kwa watoto, kuhara na malaria, aliongeza Dk. Kiula.
 
Viongozi hao walisema ingawa kituo hicho kinamilikiwa na Dayosisi ya Mpwapwa, lakini kinahudumia watu wote bila kubagua na wamekuwa wakipokea wagonjwa kutoka sehemu zote za nchi kutokana na wataalamu waliopo katika kituo hicho.
 
“Hata hivyo mahitaji yanaendelea kuongezeka siku hadi siku ndio maana tumeamua kufanya chagizo hili tuweze kujenga wodi ya wanawake, kununua vifaa vipya na pia kuongeza wataalamu,” walisema.
 
Waliongeza kuwa, ukilinganisha mahitaji ya wakati wa kuanzisha kituo hicho mwaka 1993 na mahitaji ya sasa ni wazi kuna upungufu mkubwa mno ambao wanalenga kuuboresha ili kukidhi viwango vya sasa kama ilivyoelekezwa kwenye muongozo wa “ quality of care” wa kimataifa  na “Big Result Now” wa kitaifa.
 
Kwa bahati nzuri na kwa jitihada za uongozi wa kituo na Dayosisi kwa ujumla, kituo cha Afya cha St Lukes kwa miaka miwili mfululizo, 2016 na 2017 kilichaguliwa kuwa kituo bora cha afya cha kwanza kiwilaya kwa ubora kupitia tafiti ya Matokeo Makubwa Sasa yaani “ Big Results Now” chini ya Ofisi ya Rais.
 
Walisema mgeni rasmi katika harambee hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam Julai 26, 2019 ni Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye ataongozana na viongozi wengine kutoka nje na ndani ya Mpwapwa.
 
Kwa mujibu wa viongozi hao, tayari michango mbalimbali imeanza kuwasilishwa ili sehemu kubwa ya fedha ziwe zimeshakusanywa kufikia Julai.” Tunatoa rai kwa Watanzania wote wachangie katika suala hili la kijamii ili tuweze kuokoa maisha ya wanawake na watoto na kuboresha afya zao kwa ujumla,” taarifa yao ilieleza.
  
“Tuna imani kuwa mwitikio utakuwa mkubwa ili tuweze kutimiza malengo haya kwa muda tuliojiwekea. Ni matumaini yetu kuwa kila Mwanampwapwa atashiriki kwa namna moja au nyingine maana lazima tuanzie nyumbani kwanza kabla hatujabisha hodi kwa jirani,” walisema.
 
Walisema, kampuni ya Ernegia Limited ya Dar es Salaam imeteuliwa kusimamia shughuli yote ya usimamizi na uendeshaji wa kukusanya michango hadi hitimisho la siku ya harambee tarehe 26.07.2019 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Kikwete.
 
Wametoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika, kampuni, viongozi, wafanya biashara na wanaMpwapwa wote kutoa ushirikiano na kuunga mkono katika juhudi za upatikanaji wa fedha zilizokusudiwa.

Habari Kubwa