Wachimbaji dhahabu wanane wafa shimoni

12Mar 2023
Romana Mallya
Geita
Nipashe Jumapili
Wachimbaji dhahabu wanane wafa shimoni

WACHIMBAJI wadogo wanane kati ya tisa wa dhahabu waliokuwa wanachimba madini hayo kwenye Kijiji cha Igando, Kata ya Magenge wilayani Geita, wamepoteza maisha baada ya shimo walilokuwa wanachimba kujaa maji ya mvua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo vilivyotokea usiku wa kuamkia jana.

Alisema vifo hivyo vimetokana na mvua inayoendelea kunyesha mkoani humo.

Kamanda Safia alisema kuwa eneo hilo ni lenye leseni ya utafiti na wachimbaji wadogo wanapoona hivyo, walivamia na kuanza kuchimba bila kufuata utaratibu.

"Taarifa hii ya kuwapo wachimbaji hao tuliipata usiku wa kuamkia leo (jana) majira ya saa tisa, tulipopata taarifa tulifanya vikao na diwani wa Magenge, Wilaya ya Geita.

"Wachimbaji wa Magenge walielewa na kuacha kabisa kuvamia eneo hili lakini hawa wa Iparamasa wakawa wanaingia usiku na kuanza kuchimba. Kwa bahati mbaya jana mvua ilinyesha na maji kuingia kwenye hayo mashimo, jumla yao walikuwa tisa," alisema.

Kamanda alifafanua kuwa mmoja wao alitoka kutoa mchanga juu ndipo alipoona maji yanaingia shimoni na wakati anarudi ili kuokoa wenzake ilishindikana.

"Huyu ndiye aliyetoa taarifa kwa wachimbaji wenzake wadogo kuwapo kwa wenzake chini. Kwa kuwa waliingia pale kwa jinai, hawakutoa taarifa polisi, tukio la tangu saa tisa tumekuja kulipata saa 10 alfajiri ya leo (jana) ndipo juhudi za kuwaokoa zikaanza.

"Mpaka asubuhi leo (jana) walipatikana saba na jioni hii tumempata mmoja kwa ushirikiano na Kikosi cha Zimamoto Mkoa wa Geita, jumla waliofariki dunia ni wanane na mmoja aliyetoa taarifa amekimbia," alisema.

Kamanda huyo alisema kuwa wote waliofariki dunia ni kutoa Kijiji cha Iparamasa na umri wao ni kati ya miaka 25 na 53.

"Wito wetu kwa wachimbaji wadogo wasijihusishe na shughuli za uchimbaji kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwa, serikali imewapa maeneo mengi ya uchimbaji, wakitaka kuchimba, wafuate utaratibu ili maafa kama haya yanapotokea yasiwe kwa kiasi kikubwa kama hiki," alisema.

Habari Kubwa