Wachimbaji wadogo nao wadai kuathirika

03Apr 2020
Na Mwandishi Wetu
Shinyanga
Nipashe
Wachimbaji wadogo nao wadai kuathirika

ATHARI za mlipuko wa ugonjwa wa corona zimeanza kuonekana kutokana na wanunuzi wa almasi kutoka vikundi vya wachimbaji wadogo vinavyoendelea na marudio ya makinikia ya mchanga wa madini hayo kuanza kupungua kwa kasi, hivyo wachimbaji hao kushindwa kuuza kwa wakati kama ilivyotarajiwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Shinyanga (Shirema), Gregory Kibusi, alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya uchenjuaji wa makinikia ya almasi katika Kijiji cha Msagala wilayani Kishapu, nje kidogo ya mgodi mkubwa wa almasi wa Mwadui.

Kibusi alisema kupungua kwa wanunuzi wa madini hayo kunatokana na wanunuzi wa almasi ndogondogo zenye ukubwa wa punje ya sukari kupatikana nchini India lakini kutokana na nchi hiyo kukumbwa na corona, wanunuzi kutoka nje hasa India hawaji tena.

Kuhusu malalamiko wachimbaji wadogo juu ya ubora wa mchanga huo, Kibusi alisema upatikanaji wa mchanga ambao ni takribani tani milioni moja, utaendelea kutolewa na mgodi kwa kuwashirikisha viongozi wa Shirema na kuwataka wachimbaji hao kuwa na subira.

Aliongeza kuwa pamoja na changamoto zilizopo, tayari makundi sita yanayoundwa na vikundi 100 yanaendelea na uchenjuaji wa makinikia na yanaendelea kupata almasi ndogondogo na hadi sasa wamekusanya vipande 630 na wanatarajia kuendelea kupata vipande zaidi.

Naye Ofisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Bariki Munuo, alisema wachimbaji wanapata madini lakini yanahifadhiwa na ofisi ya madini mkoa kutokana na madalali kukosa mitaji jambo ambalo linachangiwa na janga la corona.

Pia alisema kiwango cha madini hayo ni kidogo kwa kuwa kikundi kinaweza kuchenjua kiwango kikubwa cha mchanga na kupata kipande kidogo sana cha almasi na wakati mwingine kukosa kabisa.

Na changamoto nyingine wanapofanikiwa kupata mzigo unawekwa ndani wasijue ni lini watafanikiwa kuuza kutokana na ufadhili wa watu wa nje kupunguza ufadhili kwa madalali wa madini.

Simon Malila, ambaye ni mchenjuaji wa makinikia ya almasi, amepongeza mpango wa serikali kufanikisha jambo hilo na pia hakusita kuomba kupatiwa mchanga unaofaa zaidi.

Habari Kubwa