Wachimbaji waomba huduma ya majisafi

24Nov 2020
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Wachimbaji waomba huduma ya majisafi

WACHIMBAJI wadogo katika mgodi wa Kabela Gold Mine katika Kata ya Zongomela, Halmashauri ya Kahama Mjini, wameiomba serikali kwa kushirikiana na uongozi wa mgodi huo kuwapelekea huduma ya majisafi na salama ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji.
 

Waliyabainisha hayo wakati wakizungumza na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti vilivyofika mgodini hapo kuangalia namna shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini unavyoendelea, na uongozi unavyoshiriki katika kupeleka huduma za maendeleo katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
 
Lameck Japani, katika mgodi kuna ukosefu huduma ya maji ya uhakika na kusababisha kununua dumu moja la lita 20 kwa Sh. 1,000 hadi 1,500 kwa ajili ya kuoshea mawe yanayosadikika kuwa na madini.
 
Alisema kabla ya kupelekewa huduma ya nishati ya umeme pia walikuwa wakitumia gharama kubwa (majenereta) katika uendeshaji wa mgodi hasa wakati wa kuvuta maji ndani ya madura ya kuchimbia dhahabu, lakini baada TANESCO kuwafungulia huduma hiyo, gharama zilipungua.
 
Naye Yusta Kisuma, alisema wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye uendeshaji hasa wakati wa kuosha mawe yanayosadikika kuwa na dhahabu kwa kutumia maji mengi, ambayo upatikanaji wake ni shida, lakini mwisho wa siku wamekuwa wakipata ujira kidogo ukilinganisha na kile walichotumia.

Mwenyekiti wa mgodi huo, Joseph Nalemi, alithibitisha kuwapo kwa ukosefu wa huduma ya maji ya kutosha na kwamba kila siku amekuwa akitoa shilingi 20,000 kwa ajili ya kuchota maji ambayo yanatumika kwenye vyoo ndani ya mgodi ili kuviweka katika hali ya usafi na kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
 
Alisema kwa sasa huduma ya maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA) yameshafika Kata ya Zongomela na kilichobaki ni ulazaji wa mabomba ya maji na kufika katika maeneo ya mgodi.
 
Hata hivyo, Nalemi aliwataka KUWASA kuangalia namna ya kuyafikisha maji kwenye eneo la mgodi ili kuongeza kasi ya uzalishaji na uchumi wa kila mchimbaji na kulipa kodi za serikali kwa wakati, kwa kuwa na uzalishaji utaongezeka na fedha zitapatikana kwa urahisi.
 

Habari Kubwa