Wadaiwa sugu ardhi kufutiwa umiliki

26Jan 2021
Munir Shemweta
Simiyu
Nipashe
Wadaiwa sugu ardhi kufutiwa umiliki

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, amewaagiza maofisa ardhi katika halmashauri nchini kuanza kuwafutia umiliki wa ardhi wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango wa ardhi kwa mujibu wa sheria.

Mmiliki yeyote wa ardhi anapaswa kulipa kodi ya pango la ardhi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa masharti ya umiliki kwa mujibu wa kifungu 33 (1) cha Sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999.

Pia kifungu cha 48(1) (g) kinaelekeza kuwa kodi ya ardhi isipolipwa kwa kipindi cha miezi sita baada ya mmiliki kutumiwa ilani ya madai, mmiliki huyo anaweza kufutiwa milki yake.

Akiwa katika ziara ya siku moja katika Mkoa wa Simiyu, Januari 25, kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi na kuzungunza na watendaji wa sekta ya ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi aliwaelekeza wataalamu wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanatekeleza matakwa hayo ya kisheria Na 4 ya mwaka 1999 kwa kuisimamia vyema.

"Nawaagiza maofisa ardhi katika halmashauri zote kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake na msiendelee kuwalea wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi na mzingatie sheria Na. 4 ya ardhi wakati mnatekeleza majukumu yenu ikiwamo kufuta umiliki baada ya miezi sita kwa wadaiwa," alisema.

Aliwataka wenyeviti wa mabaraza ya ardhi ya nyumba na wilaya kutekeleza majukumu yao kwa kusaidia kuharakisha usikilizaji mashauri ya wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi ili kutoa haki kwa haraka.

"Hatuhitaji watu wapelekwe kwenye mabaraza ya ardhi ya nyumba na wilaya halafu mashauri yakae huko kwa miaka mitano tunataka mashauri yaishe haraka kwa mujibu wa sheria," alisema.

Vile vile, amewataka wakurugenzi katika halmashauri za Mkoa wa Simiyu kuzitumia vyema idara za ardhi katika masuala yote yanayohusu ardhi ikiwamo upangaji wa miji.

Alisema mamlaka za upangaji miji ziko chini ya halmashauri hizo na kusisitiza kuwa wakurugenzi hao wasipozitumia vyema kuna hatari ya kuendelea kwa ujenzi holela.

Pia Dk. Mabula ameonyesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi katika Mkoa wa Simiyu kwa kukusanya Sh. 87,654,120 sawa na asilimia 24, huku mkoa ukidai zaidi ya Sh. bilioni 5.5 kutoka kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ardhi katika mkoa huo, Simiyu Mwakatumbula, alimweleza Dk. Mabula kuwa ofisi yake itahakikisha inaongeza kasi ya kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ili iweze kukusanya madeni na kufikia malengo ya makusanyo ya kodi iliyojiwekea.

Hata hivyo, alisema pamoja na jitihada za mkoa kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya ardhi wanalipa, kuna changamoto kwa baadhi ya taasisi kutoonyesha jitihada zozote za kulipa na kutolea mfano wa VETA, SIDO na SHIRECU.

Habari Kubwa