Wadaiwa sugu wa NHC kuondolewa mwezi ujao

30Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
Wadaiwa sugu wa NHC kuondolewa mwezi ujao

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC)  linatarajia kuanza kuwaondoa wapangaji wa nyumba zake ambao ni wadaiwa sugu kuanzia mapema mwezi ujao.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, wakati akizungumza na wapangaji wa shirika hilo jijini Mwanza ukiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi kukagua utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi  na NHC pamoja na kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za ardhi.
 
Kwa mujibu wa Dk. Mabula, NHC inadai takriban Sh. bilioni 26 kwa wapangaji wa nyumba zake jambo alilolieleza linachangia kuzorotesha kasi ya utendaji kazi wa shughuli za kila siku za shirika ukiwamo ukarabati. 
 
“Tutachofanya sasa, yeyote aliyelimbikiza deni na tushampa notisi, lakini bado halipi kodi basi zoezi la kumwondoa litafanyika bila hata kumtaarifu upya,” alisema Dk. Mabula.
 
Aliongeza kuwa, operesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu wa nyumba za NHC itaenda sambamba na kuwaondoa wapangaji wote wasio waaminifu waliopangisha nyumba za shirika kwa gharama nafuu, huku nao wakipangisha watu wengine kwa gharama kubwa ambapo alikielezea kitendo hicho ni kuiibia serikali na halikubaliki kwa kuwa ni kosa kisheria.
 
Aliwahakikishia wapangaji wa nyumba za NHC kuwa, shirika hilo limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake ikiwa ni mpango wake wa miaka mitano na tayari kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 50 kimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, aliliomba shirika hilo kuona namna ya kuzifanyia marekebisho baadhi ya nyumba zake hasa upakaji upya wa rangi baada ya serikali kuwapanga upya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga maeneo ya miji ili kupendezesha mji.
 
Naye Meneja wa NHC  Mkoa wa Mwanza, Fadhili Anyegile, alisema, kwa mwaka wa 2021/2022  shirika hilo limeweka mikakati ya kuhakikisha linapunguza malimbikizo ya madeni ya wapangaji kwa asilimia 100 kutoa elimu kwa wapangaji juu ya utaratibu wa kulipa kodi kwa wakati na kuendelea na zoezi la kufanya matengenezo makubwa na madogo katika nyumba zake ili kuzifanya kuendelea kuwa imara.
 

Habari Kubwa