Wadau wa mazingira waomba tathimini mradi bomba la mafuta

20Oct 2021
Grace Mwakalinga
Nipashe
Wadau wa mazingira waomba tathimini mradi bomba la mafuta

WADAU wa Mazingira nchini, wameiomba Serikali kuendelea kufanya tathimini ya kutosha juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na madhara yanayoweza kutokea baada ya kukamilika na kuanza kutumika kwa mradi wa bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga.

Sambamba na hilo wadau hao wameiomba Serikali kuwalipa fidia wakazi wote waliopisha mradi huo ili kupata makazi na maeneo ya kuendeleza shughuli zao za kilimo na ufugaji.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Taasisi ya Green Faith International nchini Tanzania, Baraka Lenga  amesema  tafiti zinaonyesha  zaidi ya asilimia 90 ya mabadiliko ya tabia nchi yanasababishwa na shughuli za kibinadamu ambazo zinachangia  ongezeko la gesi  joto duniani.

Amesema utafiti huo uliofanywa na jopo la wanasayansi  wa  kimataifa  wanaoshughulika na suala la mabadiliko ya tabia nchi,  Intergovernmental Panel on Climate Change  (IPCC) wanadai miongoni mwa mambo yanayosababisha ongezeko la gesi  joto ni  nishati.

“Tanzania na Uganda kuna mradi wa bomba la Mafuta ghafi  unaendelea  kwa  kuwa nasi ni  wadau muhimu wa  mazingira tulitembelea eneo la mradi huo  jijini Tanga  kuangalia ni kwa namna gani mradi huo utakuwa na manufaa kwa wananchi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuangalia ni kwa namna gani wananchi wanaweza kuathirika na kutoa ushauri wa namna bora ya kuepukana na athari za kiafya na kimazingira,”amesema Lenga.

“Miongoni mwa mambo tuliyoyaona   kwa wananchi waliopisha mradi huo wengi wao  wamechukuliwa ardhi ambayo walikuwa wakiitumia kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji na kwamba fidia waliyoipata hawajaridhishwa nayo,” anaongeza Lenga.

Aidha baadhi ya wananchi walihojiwa wanasema walilipwa  fidia za kupisha mradi huo na wengine bado wanadai stahiki hiyo hakidhi kupata  eneo lingine kwa ajili ya makazi na kuendesha shughuli za uzalishaji mali.

Lenga amesema licha ya mradi huo kuendelea kufungua fursa za ajira kwa wananchi na kuinua uchumi kwa wafanyabiashara lakini  ni muhimu kukazingatiwa suala la mabadiliko ya tabia nchi  kwa sababu kuna miti iliyofyekwa ambayo kimsingi inasaidia  kufyonza gesi joto ambayo huitwa hewa ukaa ambayo ikiongeza katika anga hewa inaenda kuathiri  mfumo wa hali ya hewa na kusababisha ongezeko la joto duniani.

Miongoni mwa wananchi wa  Kijiji cha Chongoleani ambaye pia ni Mwakilishi wa Kanisa la Katoliki   amesema licha ya mradi huo kutoa fursa za kiuchumi  ombi lao ni kulipwa fidia ambayo itakidhi mahitaji ya kuweza kuhamia sehemu nyingine kwani  mashamba yao yalichukuliwa kwa  fidia ndogo na haikidhi kununua mashamba mengine.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Yoweri Museveni wa Uganda mwezi April mwaka huu  wamesaini rasmi mkataba wa utekelezaji wa mradi wa  kujenga bomba la mafuta ghafi kutoka Magharibi mwa Uganda hadi bandari ya Tanga Tanzania.

Mradi huo una  thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5  na umbali wa kilomita 1,440  utapita kwenye mikoa 8 ya Tanzania bara huku ukitarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36  na kuzalisha ajira takriban 15,000.

Habari Kubwa