Wadau wa ukatili waiomba Serikali kubadilisha lugha fomu ya PF3

12Aug 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Wadau wa ukatili waiomba Serikali kubadilisha lugha fomu ya PF3

Wadau wa kupinga ukatili dhidi ya watoto waiomba Serikali kubadilisha lugha inayotumika katika fomu ya PF3 kuwa ya Kiswahili na kuruhusu muuguzi wa afya (nesi) kusaini fomu hiyo ili kuleta ,haki,uelewa kwa wananchi pindi wanapopatwa na majanga.

Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence, Anitha Samson ambaye pia ni mdau wa kupinga ukatili, anasema  PF3 ni fomu muhimu wakati wa mtu kupata matibabu na kusaidia katika kesi za jinai kama vile kubakwa, ajali na vitu vingine hivyo wanaiomba Serikali kubadili fomu zote zinazohusiana na jamii ziwekwe katika lugha mama ya Kiswahili ili kila mtu aweze kuielewa.

Alisema pia ipo haja elimu kwa jamii ikatolewa ili kupata uelewa na kutambua umuhimu wa fomu hiyo sambamba na kuiweka uwazi kwani fomu hiyo umsaidia kumthibitishia daktari kumtibu mhanga kama ni tukio la ubakaji ama ajali pamoja na kumsaidia majeruhi kuwa na ushaidi kisheria hasa kesi yake itakapo fikishwa Mahakamani.

"Serikali idara ya Polisi wafanyemabadiliko kama wanaweza kufanya mabadiliko kwenye nyaraka  mbalimbali wanashindwa nini kufanya kwenye hii PF3 ambayo ina kurasa mbili hivyo ni vyema wakafanya marekebisho ili wananchi waweze kuelewa kilichoandikwa pamoja na kuona umuhimu wa nesi kujaza fomu hiyo kwani wao ndio wapo hospitalini muda wote tofauti na madaktari " alieleza Samson.

Meneja  Mradi wa Boresha (TIP) Wilaya ya Ilemela Dk. Pestory Mondea.

Meneja  Mradi wa Boresha (TIP) Wilaya ya Ilemela Dk. Pestory Mondea, alisema  kutokana na maelekezo kumtaka daktari ajaze fomu hiyo lakini kuna umuhimu wa mtumishi kujaza ili kutopoteza ushahidi pindi tukio la unyanyasaji wa kingono litakapotokea.

"Kwa sasa tunahamasisha ili hata manesi wapatiwa fursa ya kuweza kujaza fomu hiyo ya PF3 ili  kumpatia mhanga matibabu mapema mfano aliyebakwa aweze kukingwa na maabukizi ya virusi vya UKIMWI ambayo anatakiwa apate ndani ya masaa 74."alieleza Dk. Mondea.

Naye Kasomi Kazimili mkazi wa Mecco wilayani Ilemela alisema adha anayoipata kutokana na kutokuwa na uelewa na fomu ya PF3 ni ukosefu wa elimu kwa wananchi na kutaka na fomu hiyo iwe wazi kwani itasaidia mtu kutambua nini kilichoandikwa ili kutokuleta udanganyifu .

"Lugha inayotumika kwenye PF3 inatakiwa kuwekwa katika mfumo wa kiswahili ili kusaidia mhanga wa tukio husika kufahamu ni nini daktari amekiandika kama kinaendana na uhalisia wa tukio kwani wahanga wengi wa vitendo vya ukatili ni watoto na wakati mwingine unakuta mzazi wake hajui kusoma ila kama imeandikwa kwa lugha ya kiswahili na mwandiko unaosomeka ni rahisi hata kwa kwa mtoto ambaye ni mwanafunzi kumsomea na kuelewa kilicho andikwa."alisema Salvatory Joseph, Mkazi wa Mecco 

Aidha Mwanasheria wa Shirika la Tanzania Interfaith Partnership (TIP)Suzana Mwaitenda, alisema Serikali inapaswa kuongeza muongozo wa majukumu ya ziada ambayo amepewa muhudumu wa afya itasaidia hasa kwa manesi pia wizara husika itakapokubali wao watatoa elimu kwa manesi wote kuhusiana na ujazaji wa fomu namba tatu ya Polisi .

Habari Kubwa