Wadau wa mazingira wazindua kampeni ya PlastikiNoma

15Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau wa mazingira wazindua kampeni ya PlastikiNoma

KATIKA kuunga juhudi za serikali katika kuhamasisha kuacha matumizi wa vifaa vya plastiki, wadau wa mazingira wanatarajia kuzindua kampeni iitwayo "PLASTIKI NOMA" itakayofanyikwa Julai 18 mwaka huu kwa kufanya usafi kwenye eneo la Daraja la Selander jijini Dar es Salaam.

Dk. Vicencia Shule akizungumza na waandishi wa habari.

Akizungumza leo jijini, Dk. Vicencia Shule, alisema kuwa kampeni hiyo inatarajia kushirikia wadau mbalimbali wa mazingira kutoka Manispaa zote tano za Dar es Salaam pamoja na vijana 150 kutoka katika Kituo cha Baba Watoto ambacho kinalea watoto mbalimbali wa mitaani.

Dk. Shule alisema kuwa wamefikia kuzindua kampeni hiyo ambayo itakuwa endelevu baada ya kufanya utafiti kwenye Bahari ya Hindi na kubaini athari mbalimbali zinazotokana na takataka za plastiki ambazo huchelewa kuharibika.

Alisema kuwa utafiti wao ambao ulianza Septemba mwaka jana na utakuwa ni wa mwaka mmoja, utalenga kutoa elimu kwa jamii na hasa vijana kuhusu madhara yanayopatikana baada ya kutumia bidhaa za plastiki.

"Utafiti wetu tumechagua kuufanya kwenye eneo la ufukwe wa Bahari ya Hindi, tunatarajia kutoa elimu ambayo itasaidia kuifanya jamii kupambana na takataka za plastiki, tukilenga madhara wanayopata viumbe kama samaki na mimea, ukweli ni kwanza taka hizi haziozi, ni ngumu sana, tuandae mfumo mzuri wa kuteketeza taka hizo," alisema Dk. Shule.

Alieleza kuwa katika utafiti wao waliwashirikisha wavuvi, wanafunzi, madereva mbalimbali wa magari na makundi ya vijana wakiwamo wa Kituo cha Baba Watoto ambao wanatumia sehemu ya takataka hizo kutengeneza vitambaa na sanaa.

Naye Kiongozi wa Utafiti, Dk. Rose Masalu, alisema kuwa moja ya njia rahisi ya kutokomeza takataka hizo za plastiki ni kuzisaga na kutumia unga unaopatikana kutengeneza maligafi mbalimbali kama mikoba ya wanawake na viatu.

Alisema kama nchi, baada ya katazo ya kutumia mifuko ya plastiki, mji umeanza kuwa msafi na anaipongeza serikali kwa kutoa mwongozo wa kuachana na bidhaa hizo.

Aliongeza kuwa licha ya Tanzania kuchelewa kutoa agizo la kutumia mifuko ya plastiki ukilinganisha na nchi jirani zinazotuzungumza ikiwamo Uganda ambao walisitisha matumizi hayo tangu mwaka 2007, mapokeo yamekuwa ni makubwa zaidi.

Habari Kubwa