Wadau wa ngozi kutumia fursa kiwanda cha kuchakata ngozi

11Aug 2020
Dotto Lameck
Dodoma
Nipashe
Wadau wa ngozi kutumia fursa kiwanda cha kuchakata ngozi

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, amewataka wadau wa ngozi nchini kutumia fursa ya kiwanda cha kuchakata ngozi kinachojengwa Jijini Dodoma kwa lengo la kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na ngozi.

Manyanya ametoa rai hiyo alipofanya ziara ya kukagua mradi huo unaotekelezwa katika eneo la Zuzu lililopo jijini  humo.

Manyanya amesema wadau wa ngozi wanapaswa kujitathmini na kuhakikisha ngozi zinafikishwa pale kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na ngozi baada ya mradi huo kukamilika.

“Sisi matarajio yetu , serikali itatenga fedha kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati hivyo wadau  tunataka tushirikiane katika dira hii ili kufanya kitu cha uhakika na kuhakikisha viatu na bidhaaa nyingine zinazopatikana kwenye ngozi zinakuwa zinazalishwa hapa nchini” 

“Niwatake wadau wa sekta ya ngozi kwa kuwambia kuwa mambo yameiva sasa ni wakati sasa wa kuchangamkia fursa zilizopo makao makuu ya nchi Dodoma” amesema Manyanya.

Aidha, Mhandisi Manyanya ameagiza kiwanda hicho kujengwa kwa ubora unaohitajika, kusimamiwa vizuri ili kupata jengo bora, na matumizi ya fedha yaendane na ubora wa jengo, pia linatakiwa kujengwa kwa kasi ili kuaanza kufanya shughuli zake.

Habari Kubwa