Wadau wa ushirika watoa mapendekezo 9 kuanzishwa benki yao

24Apr 2022
Godfrey Mushi
KILIMANJARO
Nipashe Jumapili
Wadau wa ushirika watoa mapendekezo 9 kuanzishwa benki yao

BAADA ya serikali kubariki rasmi mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika, wadau wa sekta hiyo nchini, wamependekeza mambo tisa wanayotaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuja na mkakati mahususi wa kisera na kimuundo ili kuijengea wigo benki hiyo isianzishwe na kufa.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Waziri Bashe, alishauriwa hayo leo na wanazuoni, wana ushirika na wabia wa maendeleo kutoa Taasisi za Fedha, wakati wa mdahalo wa kitaifa juu ya uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika, uliofanyika ili kufanya uchambuzi wa fursa na changamoto.

Akitangaza maazimio ya wadau hao, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Dk. Jones Kaleshu, amesema wanataka wakati Benki hiyo inaanzishwa, pia kuanzishwe chombo maalum kwa ajili ya kutunza hisa za ushirika, ndani ya Benki ya hiyo ya Taifa ya Ushirika.

“Tunataka kianzishwe chombo maalum kwa ajili ya kutunza hisa za ushirika ndani ya Benki ya Taifa ya Ushirika. Hicho chombo ambacho kitaanzishwa kwa maana ya Kampuni Hodhi, ikafanye kazi ya uwekezaji ili kuifanya benki hiyo ijiendeshe na kusonga mbele.

“Aidha, wadau wengi wa sekta ya ushirika, wamependekeza kuanzishwa mara moja kwa Benki ya Taifa ya Ushirika. Wanataka pia, elimu na hamasa itolewe kwa ukubwa wake kwa wanaushirika kununua hisa kuanzia sasa KCBL (kwenye Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro).

Maazimio mengine ni hisa za ushirika ndani ya Benki ya Taifa ya Ushirika, ni lazima zilindwe kwa kuweka utaratibu utakaolinda hisa hizo ili kulinda msingi wa benki.

Kwa mujibu wa Dk. Kaleshu, wadau wa sekta ya ushirika wanataka kuwepo na uwekezaji wa kimkakati ili kutumia fursa hiyo kupata mtaji wa kuendesha benki hiyo kuifanya kusonga mbele

“Lakini vilevile tunataka serikali iweke mazingira rafiki ili kuruhusu Benki ya Taifa ya Ushirika kuanzishwa na kuendelezwa; hii ni pamoja na kuanzishwa Sheria ya Ushirika ili kuruhusu mfumo kuwa hai ili kuongeza mtaji

“Elimu ya Ushirika ianze kufundishwa kwenye Shule za Msingi ili kujenga uelewa zaidi na ukuaji wa sekta ya ushirika.”

Aidha, Dk. Kaleshu, amesema wadau wa sekta ya ushirika nchini wanataka mabadiliko ya kina kutoka Benki ya KCBL, kuwa Benki ya Taifa ya Ushirika yafanyike ili kuruhusu watu wengi kununua hisa.

Limo pia pendekezo la kutaka vyama vya ushirika vilazimishwe kisheria kununua hisa katika Benki ya Taifa ya Ushirika.

Katika mdahalo huo, Meneja Mkuu wa Benki ya KCBL itakayobadilishwa kuwa Benki ya Taifa, Godfrey Ng’urah, amewasilisha mada kuhusu mafanikio, mikakati na muundo wa Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania, huku Dk. Mathias Nkuhi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), akitoa mada juu ya mazingira ya kisheria na kisera, Je yanawezesha uendeshaji wa kisasa wa Benki ya Taifa ya Ushirika?

Mada nyingine ni nafasi ya Benki ya Taifa ya Ushirika katika Huduma Jumuishi za Kifedha iliyowasilisha na Frank Nyabundege Kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na mada kuhusu Benki ya Taifa ya Ushirika na ushindani katika tasnia ya biashara kibenki iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB nchini, Abdulmajid Nsekela.

Habari Kubwa