Wadau waanzisha operesheni tokomeza ukatili kijinsia

08Oct 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Wadau waanzisha operesheni tokomeza ukatili kijinsia

KATIKA jitihada za kupambana na ukatili wa kijinsia uliojikita wilayani Rorya mkoa wa Mara, wadau na watetezi wa haki za binadamu wameanzisha kampeni ya tokomeza ukatili.

Asasi ya kiraia ya kisheria inayojishughulisha na masuala ya kisheria na kijamii mkoani hapa ndiyo inatekeleza mradi wa kupiga vita na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, imani potofu na mila chochezi kwa wana-Rorya.

Mradi huo umelenga kufikia watu 100,000 kwa kipindi cha miezi sita kwa gharama ya Sh. milioni 60 kazi inayofanywa kwa kushirikiana na shirika la Foundation For Civil Society.

Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya msaada wa kisheria Ostack Mligo, alisema hayo wakati akizungumzia na waandishi wa habari mjini Musoma na kuongeza kwamba mradi huo ni endelevu na kwa kuanza utafanyika ndani ya mwaka mmoja.

Alisema utekelezaji wa mradi huo wilayani hapa unafuatiwa na vitendo vya kikatili vinavyofanywa dhidi ya watoto,wanawake, wanaume,watu wenye ulemavu pamoja na wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

"Kwa mujibu wa mkutano uliofanywa na jamii wilayani Rorya vyanzo au visababishi vya ukatili huu ni kukumbatia mila na desturi zilizopitwa na wakati kama kuacha kazi za uzalishaji mali mpaka tendo la ndoa lifanyike kwanza wakati wa mavuno au msimu wa kuandaa mashamba"alisema.

Mwanasheria huyo alieleza kuwa jambo hilo limesababisha kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana kujamiiana ikiwa ni pamoja na kuenea kwa maambukizo ya VVU na Ukimwi kwa wananchi wilayani hapa.

Alisema ukatili ambao unaonekana kuwa wa hali ya juu ni ukatili wa kiuchumi ambapo wanawake wanapigwa na wananyimwa haki ya kumiliki mali kama vile mashamba lakini hawana haki ya kurithi rasilimali ambayo imeachwa na mume . Lakini pia hupigwa , watoto nao hushambuliwa na hata watu wa makundi maalum nao wanaonewa.

Mligo alisema ili kuondoa tatizo hilo wilayani hapa kwanza kupitia mradi huo shirika hilo linatarajia kufanya majadiliano ya kutambua chanzo cha matukio hayo kikao kitakacho shirikisha wazee wa mila, viongozi wa serikali za mtaa, Mahakama na jeshi la polisi ,kuangalia jambo lililopo ndani ya jamii hiyo.

"Pia tutawajengea uwezo vyombo vya utatuzi wa migogoro ambapo ni pamoja na mabaraza ya kata katika ngazi ya vijiji , kata mahakama na polisi kwani hawa wote wanahusika na mambo ya ukatili wa kijinsia kwa hiyo tunawafundisha taratibu na misingi inayotakiwa wakati wa kutatua hii migogoro,’’alisisitiza.

Alisema mradi huo utatekelezwa katika kata 13 zilizopo wilayani Rorya huku akitaja kata sita ambazo zimeshaanza kufikiwa na mradi huo kuwa ni Nyamtinga, Nyamagaro, Mirare,Kyangasaga,Kinyenche, Raranya na Roche.

Habari Kubwa