Wadau wachangia mil. 30/- ununuzi wa mashine tiba

03Oct 2021
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Wadau wachangia mil. 30/- ununuzi wa mashine tiba

DIWANI wa Kawe mkoani Dar es Salaam, Mutta Rwakatare, ameishukuru Rotary Club Tawi la Mbezi Beach kwa kuendesha kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya matibabu katika Zahanati ya Kawe.

Club hiyo imelenga kuchangisha Sh. milioni 90 kwa awamu tatu kwa ajili ya kununua vifaa vya matibabu ikiwamo mashine ya Utra Sound na gari la kubebea wagonjwa.

Rwakatare, akizungumza jana muda mfupi baada ya kumalizika kwa michezo mbalimbali ya kuhamasisha uchangiaji huo, alisema kuchangishwa kwa fedha hizo kutasaidia kuokoa maisha ya watu wengi wanaokosa huduma muhimu katika zahanati hiyo.

"Ninaishukuru Rotary Club ambao ni wadau wetu wakubwa wa maendeleo wanaotusaidia katika Sekta ya Afya. Kuwapo kwao leo hapa kutasaidia kukusanya fedha kwa ajili ya kununua mashine ikiwamo ya Ultra Sound ili kusaidia wananchi kupata vipimo katika zahanati hiyo,” alisifu.

Rais wa Rotary Club, Pamela Mutabasi, alisema kupitia michezo waliyoshiriki jana, walilenga kukusanya Sh. milioni 30 ili kuchangia vifaa vya matibabu katika zahanati  hiyo.

Alisema katika club yao wameweka vipaumbele viwili katika Shule ya Msingi Kawe na Zahanati ya Kawe kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

“Fedha hizi ambazo tunachangisha leo (jana) hapa zitasaidia kununua mashine tatu za kutolea huduma katika Zahanati yetu ya Kawe ikiwamo mashine ya Ultra Sound.

“Awamu ya pili tunatarajia kukusanya tena Sh. milioni 30 na baadaye awamu ya tatu tutamalizia kukusanya tena kiasi hicho cha fedha," alisema.

Alisema Rotary ni mtandao wa kimataifa unaojumuisha majirani, marafiki na viongozi na kwamba wamekuwa wakifanya kazi za kujitolea kwa jamii kwa zaidi ya miaka 110 katika sekta za elimu, afya, maji, kudumisha amani, afya ya mama na mtoto pamoja na kukuza vipato kwa wenye vipato duni.

Habari Kubwa