Wadau walia sheria ya ajira kwa walemavu kutotekelezeka

24Sep 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wadau walia sheria ya ajira kwa walemavu kutotekelezeka

WADAU wa masuala ya watu wenye ulemavu, wameilalamikia sheria ya ajira ya watu wenye ulemavu ya mwaka 1982, ambayo inasema asilimia 3 ya wafanyakazi wawe watu wenye ulemavu, kuwa imekuwa haitekelezwi ipasavyo.

Hayo yamebainishwa Jana kwenye mafunzo yaliyohusisha waandishi wa habari na mashirika yasio ya kiserikali kutoka mikoa mbalimbali, yaliyokuwa na lengo la kuandika habari za watu wenye ulemavu ambayo yaliandaliwa na Shirika la Internews.

Akitoa mafunzo ya sheria za watu wenye ulemavu kwa waandishi hao wa habari, Mwanasheria Novathy Lukwago kutoka Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA makao makuu, amesema sheria ya ajira ya watu wenye ulemavu ya mwaka 1982 imekuwa haitekelezwi ipasavyo kuajiri watu hao.

“Sheria hii ya ajira ya watu wenye ulemavu ya mwaka 1982 imekuwa haitekelezwi ipasavyo, sababu hakuna muongozo wa ufuatiliaji ambapo sheria hii inapaswa kuundiwa timu ya kufuatilia kuajiri watu wenye ulemavu, pamoja na Kamishina wa Ajira awe anapeleka taarifa bungeni kila mwaka ili kufanya Tathimini,” amesema Lukwago.

Nao baadhi ya waandishi wa habari ambao walihudhulia kwenye mafunzo hayo, wamesema wanapokuwa wakiandika habari zao juu ya watu wenye ulemavu, baadhi ya changamoto kubwa ambazo hukumbana nazo kwao ni ukosefu wa ajira, ambapo sheria hiyo imekuwa haitekelezwi, na wao kuendelea kukabiliwa na ugumu wa maisha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) mkoani Shinyanga Richard Mpongo, akizungumza na Nipashe, ameiomba serikali kupitia Wizara husika ya watu wenye ulemavu, kuisimamia sheria hiyo kwa vitendo, ili watu hao wapate ajira na kujikwamua kiuchumi.

Naye Mratibu wa mafunzo kutoka Shirika la Internews Shabani Maganga, amesema wameendesha mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari, ambao wamekuwa na mchango mkubwa wa kutatua changamoto mbalimbali za watu wenye ulemavu kupitia kalamu zao.