Wadau waombwa kusaidia watoto mazingira hatarishi

20Jul 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Wadau waombwa kusaidia watoto mazingira hatarishi

JUHUDI za lazima zahitajika kufanyika na wadau mbalimbali za kuwasaidia watoto 54,911 wa Mkoa wa Arusha, wanaoishi kwenye mazingira hatarishi na kulelewa kwenye vituo ili waondokane na changamoto zinazowakabili.

Hayo yalisemwa jana na Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Arusha, Denis Mgiye, wakati akizungumza katika semina ya siku tatu kwa wadau wa masuala ya watoto wakiwamo wachungaji, waandishi wa habari,

na maofisa maendeleo ya jamii yaliyoandaliwa na shirika linaloshughulika na masuala ya malezi na ulinzi wa mtoto la SOS Children Villages Tanzania.

Alisema kwa takwimu za hadi Machi mwaka huu, wilaya inayoongoza kwa kuwa na watoto wengi ni halmashauri ya Jiji la Arusha ambayo ina jumla ya watoto 21,687 .

Alisema changamoto kubwa ambazo zimekuwa zikichangia kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto waishio mazingira magumu ni kuwapo kwa umaskini uliokithiri ngazi ya jamii, migogoro ya ndoa, ukatili wa kupindukia pamoja na wazazi kutowajibika ipasavyo.

Kutokana na hali hiyo, alitaka elimu zaidi kutolewa kwa jamii katika kutambua madhara yanayotokana na migogoro ya kifamilia ili kuwanusuru watoto hao.

“Endapo tutaunganisha nguvu wadau wote tutasaidia watoto hawa kuondokana na changamoto zinazowakabili,” alisema.

Mratibu Taifa utetezi wa haki za watoto wa shirika hilo, Mpelly Kalonge, alisema lengo la semina hiyo ni kusaidia watekelezaji wa sera za mtoto na wadau wa maendeleo ya mtoto kujadili changamoto zinazowakabili watoto na kutoka na suluhisho la pamoja.

Mpelly alisema kupitia semina hizo wamekuwa wakiangalia kila mdau ana nafasi gani katika kushughulikia kwa pamoja changamoto zinazowakabili  watoto na kuongeza nguvu ili kuhakikisha ukatili unaoendelea dhidi ya watoto unakomeshwa.

Aliongeza changamoto kubwa iliyopo katika jamii ni kutokuwapo kwa ushirikishwaji wa kutosha kwa mtoto katika kutoa maamuzi ndani ya jamii, hali ambayo hupelekea mtoto kutokuwa muwazi katika kuelezea changamoto anazokabiliana nazo hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia.

Mmoja wa washiriki katika semina hiyo, Salvatrix Kinabo ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto wadogo wa mchana (daycare) cha St. James Kingdom alisema kuwa, kumekuwapo na sheria zinazomlinda mtoto ila changamoto iliyopo ni kuwapo kwa usimamizi hafifu katika sheria hizo.

Aliwataka wadau mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla kuona suala la kumlinda mtoto ni la kila mmoja, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kusimama

katika nafasi yake kuhakikisha wanatokomeza changamoto zinazochangia kuwapo kwa watoto wa mitaani na kukomesha suala zima la ukatili wa kijinsia.