Wadau wapewa neno utunzaji rasilimali maji

16Jul 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau wapewa neno utunzaji rasilimali maji

OFISA wa Maji Bonde la Wami Ruvu, Simon Ngonyani, amesema changamoto kubwa iliyopo sasa nchini ni upatikanaji wa maji ambayo ndio ‘injini’ ya maendeleo kuelekea Tanzania ya viwanda, hivyo wadau wa maendeleo pamoja na serikali wanapaswa kuunga mkono juhudi za utunzaji wa rasilimali za maji.

OFISA wa Maji Bonde la Wami Ruvu, Simon Ngonyani,akiwasilisha mada katika mkutano wa saba wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde nchini uliofanyika Kigoma.

Ushauri huo aliutoa mwishoni mwa wiki katika mkutano wa saba wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde nchini uliofanyika Kigoma.

Ngonyani alisema changamoto kubwa kwa bodi ya maji ya Bonde la Wami/Ruvu ni uwapo wa ongezeko la viwanda katika ukanda wa bonde hilo ambao kwa namna moja ama nyingine ni watumiaji wakubwa wa maji, hivyo basi ni lazima kufanyike jitihada za kutosha kuhakikisha vyanzo vinalindwa na maji yanakuwapo.

Alisema kutokana na maji kuwa kidogo, siku za usoni kutakuwa na changamoto ya ugawaji wa maji kwa sababu watumiaji ni wengi, na maji ni kidogo, hivyo wamejipanga kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa kwa ufasaha ili kukabiliana na hali hiyo hapo baadaye.

“Embu tujiulize maswali haya; maji yapo wapi? Swali la pili; je, kwa haya maji yaliopo ni endeleavu…yataendelea kuwapo na kutosheleza mahitaji?... Swali la tatu; Je, maji yaliopo yana ubora? Tukipata majibu ya haya maswali tutaona tunatakiwa kuchukua jitihada za makusudi katika kuongeza nguvu katika utunzaji wa vyanzo vya maji,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa hali ya maji iliyopo sasa hakuna budi wakulima wakubwa na wadogo wakaachana na umwagiliaji wa mafuriko “floods Irrigation” kwani hayo ni matumizi mabaya ya maji. “Juzi tulienda kwenye kiwanda cha Sukari cha Mtibwa tulikuta wanatumia floods Irrigation kumwagilia mashamba yao ya miwa tulikuta maji mengi sana hadi yanatisha lakini tulizungumza nao na kuwaelimisha jinsi ya kutumia maji vizuri kwani wapo wenzao wa kiwanda cha sukari Bagamoyo wanatumia umwagiliaji wa matone “Drip Irrigation” kwa maana hiyo tukitumia maji kwa ufanisi yanaweza yakatosha,” alisema Ngonyani.

Aliongeza kuwa hakuna namna ambavyo serikali ikajitoa katika kusimamia rasilimali za maji kwa maana ya rasilimali kwa kuwa mabonde yanatakiwa kuwezeshwa na sio kutegemea mapato yake pekee au wadau wa maendeleo.

Alisema serikali inatakiwa kuongeza nguvu katika mabonde ili maji yaendelee kuwapo ili kesho ya Dar es Salaam iendelee kuwapo kwani kuna wakati Mto Ruvu ukipata “mafua” pampu za kusukuma maji za Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) zinaungua.

“Njia pekee ya kukabiliana na hali hiyo ni kujenga lile bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro na endapo tusipofanya hivyo tutakuwa tumegonga mwamba,” alisema.