Wadau wataka kamati mitaani kuzuia ukatili

10Aug 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau wataka kamati mitaani kuzuia ukatili

WANAWAKE na wadau wanaoshughulikia masuala ya watoto, wameomba kuundwa kwa kamati za kuzuia ukatili katika mitaa na vijiji ili kuimarisha juhudi za kupambana na vitendo hivyo nchini.

Wakizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wadau hao pia walisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanaume katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo katika jamii.

"Ni wakati mwafaka wa kuunda kamati za kupambana na vitendo vya ukatili ambavyo vinaripotiwa kukithiri kila siku katika jamii, vijiji na mitaa, na kuna umuhimu wa kuwashirikisha viongozi wa mitaa kusukuma mbele juhudi za kupambana na vitendo hivi,” alisema Malcela Lungu, Mkurugenzi wa Shirika la Mabadiliko na Kujenga Ushirikiano kwa Wote (TIBA).

Alisema ushiriki wa wanaume katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo haujaonekana, na kwamba kuanzishwa kwa kamati hizo kutasaidia kuongeza zaidi elimu ya ufahamu juu ya vitendo hivyo vya ukatili.

"Kama wadau, tunalazimika kukaa chini na kujiuliza ni jinsi gani tutafanya kazi kwa pamoja, tuimarishe juhudi za kuhakikisha kuwa tunapambana na vitendo hivi kwa nguvu zote vinavyoendelea kufanyika katika jamii.

Lungu alisema kuwa hadi sasa TIBA imefanya mipango ya uhamasishaji katika kata na mitaa mbalimbali ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na kwamba wamepanga kuendelea kutoa elimu katika maeneo mengine ikiwamo katika vikundi mbalimbali na katika makundi ya watu wanaojikusanya kwenye vibanda vya kahawa.

Michael Sungusia, mtaalamu wa mambo ya jinsia, alisema kunahitajika mipango madhubuti zaidi ya uhamasishaji katika kushughulikia suala hilo.

"Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja mpaka ifike wakati tuone juhudi na matokeo mazuri kwa jamii yetu tunayoihudumia na tunaokoa maisha ya wanawake, watoto na wasichana ambao ndio waathirika wakubwa,” alisema Sungusia.

Habari Kubwa