Wadau watoa ya moyoni sakata Kinana, Makamba

19Jul 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau watoa ya moyoni sakata Kinana, Makamba

WASOMI na viongozi wa dini wametoa maoni yao kuhusu sakata la makatibu wakuu wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba, kuliandikia barua Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa chama hicho.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wawili hao waliandika barua kwa baraza hilo lililo chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, wakilalamika kuhusu tuhuma za kumhujumu Rais Magufuli zilizotolewa dhidi yao na mtu anayejiita mwanaharakati huru.

Tayari baraza hilo limeshawajibu wawili hao, likieleza kuwa suala lao lilipaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu zilizoainishwa kwenye katiba ya chama hicho badala ya kukimbilia kwa baraza.

Akizungumza na Nipashe jana kuhusu suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa, alisema barua ya viongozi hao inaonyesha kutokuaminiana ndani ya chama hicho na kwamba viongozi hao wastaafu wameleta somo jipya kwa jamii ya sasa.

“Hii inaonyesha kutokuaminiana ndani ya chama na bahati nzuri wote ni wazee na wakati fulani ni jukumu lao kujengeana imani.

“Siijui katiba yao vizuri lakini nadhani panapotokea tatizo ni muhimu apatikane mtu wa katikati atakayesimama kama msuluhishi.

"Kwa hiyo, kuwaambia waende kwa viongozi waliopo sasa ambao ndiyo kama upande wao wa pili si sawa na hawakukosea kuileta 'public' (kwa umma) kwa sababu yule kijana (anayetuhumiwa kuwachafua) tayari aliwatuhumu hadharani," alisema.

Mhadhiri mwingine katika Idara ya Sayansi ya Siasa  ya UDSM, Dk. Benson Bana, akizungumza na Nipashe jana, aliwataka Makamba na Kinana kumwona Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli, ili kupata ufumbuzi wa suala lao.

Dk. Bana alisema njia iliyotumiwa na makatibu wakuu wastaafu wa CCM hao kuandika waraka na kuachia hadharani, haiwezi kuwapa matokeo mazuri.

"Wangemwona Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM ama watendaji wakuu wa chama na si Baraza la Wazee ama sivyo wangeenda mahakamani kama alivyofanya mwenzao Benard Membe, vinginevyo hawawezi kupata matokeo mazuri zaidi ya kujichafua zaidi na kuzidi kufedheheka," Dk. Bana alisema.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema ni mapema kuyaongelea makundi yanayoibuka lakini kunahitaji uangalifu kutokana na athari zake kwa ustawi wa nchi.

Alisema suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa haraka kwa kuwa linamgusa Rais na haijajulikana wananchi wako upande upi katika mgogoro huo.

"Kama jambo hili litaendelea katika sura hiyo, maana yake mustakabali wa chama na taifa unakuwa haukai vizuri kwa sababu Rais ni taasisi.

“Utakuwa unagusa watu wengi unapojaribu kumvunjia heshima Rais, unawagusa Watanzania wengi, hili jambo halipendezi kuachwa liendelee, umakini mkubwa unahitajika wa namna ya kuyatazama haya makundi ili yasilete athari kwa watu," alisema.

Kiongozi huyo wa dini alitoa wito kwa pande zinazohusika, kutumia hekima na busara katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza kati yao.

“Bahati nzuri wana vikao vyao vya chama na serikali ina taratibu zake za kuona namna ya kulishughulikia. Vyombo vya ulinzi na usalama navyo vichukue nafasi yake, kuna kauli inasema 'moto mkubwa huanza na cheche ndogo', hata vyombo vya ulinzi na usalama vione, visidharau yanayoendelea," alishauri.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa, alisema Makamba na Kinana wametoa tahadhari kwamba hali ikiachwa ikaendelea hivi kutaligawa taifa na kuna uwezekano mkubwa wa kuingia katika mazingira magumu ya amani na utulivu.

“Duniani kote wanaovunja amani wanaweza kuwa watu wengi au mtu mmoja anatumiwa, tuna mifano ya nchi kama Rwanda na Tunisia ambako mtu mmoja alisababisha kuingia kwenye machafuko,” alisema.

“Kinana na Makamba wamelisaidia taifa kwamba wazee wastaafu waliopo waingilie kati kwa kuwa wapo waliokwenda kwenye vyombo vya habari na mahakamani lakini hali haijabadilika.

“Kama hili la Makamba na Kinana halitaweza kutatua na kujenga mazingira ya mtu huyu kudhibitiwa kwa mujibu wa sheria ya nchi, itakuwa na tafsiri kwamba mtu mmoja asipodhibitiwa ana uwezo wa kuvunja amani na taifa likavurugika kabisa kama tulivyoona kwenye nchi nyingine.

“Kuna watu wameitwa wahaini, mawakala wa mabeberu na majina mengineyo mabaya, bado aliyetaja hayo na kuandika kwenye chombo cha habari, ameachwa na chombo anachotumia kimeendelea kuachwa bila kuchukuliwa hatua, ni kuliingiza taifa kwenye mgawanyo mkubwa.

“Ni sawa na simba anayekula nyama ya mtu na akiachwa ataendelea kula, ni tabia ambayo ikiachwa ikaendelea ni jambo baya sana. Ilipaswa kuchukua hatua toka awali lakini ameendelea kuachwa."

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, alisema tofauti za kimtazamo zilizoibuliwa na wazee hao zilipaswa kufanyiwa kazi ndani ya chama kwa kuwa wana utaratibu wao wa chama.

“Nilitegemea walioandika barua wangeomba usuluhishi na anayewasema vibaya, ungeweza kufanyika ndani kwanza kabla ya kwenda kwa umma. Sidhani kama inaelekea mahali pazuri mpasuko kwa viongozi wakubwa kama hao,” alisema.

"Inawezekana alikosea kuwasema lakini chama kingechukua hatua ikiwamo kumuonya kuliko majibizano ya barua, ni vyema kama wameshindwa kuelewana ndani, waende mahakamani.

"Nadhani wafanye usuluhishi ndani ya chama chao kwa kuwa ni kikubwa na kina mifumo ya kushughulikia mambo kama hayo. Tunahitaji amani zaidi kuliko malumbano sisi kama Watanzania,” alisema.

Wakili Hudson Ndusyepo, alisema barua ya malalamiko iliyoandikiwa na Makamba na Kinana inazua maswali  kisheria na kisiasa.

Alisema barua hiyo ingekosa vigezo kama ingekuwa inapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, akibainisha kuwa kisheria hairuhusiwi kuunganisha malalamiko ya kuvunjiwa heshima kwa kuwa kila mmoja ana heshima yake binafsi.

“Kila mmoja alipaswa kuandika malalamiko yake binafsi, lakini kwa kuwa wameiandika kisiasa, pia inaacha maswali kwanini wameamua kufikisha malalamiko yao kwenye baraza hilo, huyo wanayemlalamikia ni mwanachama, ana wadhifa gani ndani ya chama hicho?" Alihoji.

Alisema hatua iliyochukuliwa na wawili hao pia inaibua hoja nyingine kwamba huenda kuna watu wanajiita wanaharakati ilhali wana nyadhifa za siri zisizojulikana kwa jamii lakini chama husika kinawatambua.

*Imeandikwa na Enock Charles, Beatrice Moses, Romana Mallya na Salome Kitomari

Habari Kubwa