Wadau, watumishi wafurahia  kupanda viwango mishahara

16May 2022
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wadau, watumishi wafurahia  kupanda viwango mishahara

WADAU na watumishi wa serikali wamepongeza uamuzi wa serikali wa kupandisha mishahara huku wakisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametekeleza ahadi yake siku ya Mei Mosi, mwaka huu kwa vitendo.

Juzi, Rais Samia, aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ikiwamo kima cha chini kwa watumishi wa umma kuwa kwa asilimia 23.3, huku ikielezwa Sh. trilioni 1.59 zitatumika katika ongezeko hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, ilisema serikali imepanga kutumia Sh. trilioni 9.7 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika serikali kuu, serikali za mitaa, taasisi na wakala za serikali.

Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema uamuzi huo ni mwendelezo wa hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya CCM awamu ya sita.

“Tayari serikali ilishapunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi nane, kufuta tozo ya kulinda thamani ya mkopo ya asilimia sita (Value Retention Fee) kwa wanufaika wa mikopo elimu ya juu wakati wa marejesho na upandishwaji wa madaraja kwa kuzingatia miundo ya utumishi wa kada mbalimbali,” alisema Shaka.

Aliongeza kuwa hatua zote hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025, ibara ya 130, ukurasa wa 180-181.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe, Scolastika Kevela, alipongeza  na kusema imeonyesha jinsi Rais Samia alivyo mlezi mzuri kwa wafanyakazi wake.

Hapiness John mkazi wa Mbezi Makabe, alisema uamuzi wa Rais kuridhia nyongeza ya mshahara umekuja wakati mwafaka kutokana na vitu kupanda bei mfululizo hivyo itasaidia kupunguza gharama za maisha.

“Rais amekuwa kama mkombozi katika kipindi hichi, hicho alichokiongeza sio kwamba kitamaliza shida zetu, ila kitapunguza mzigo wa maisha kwa kiasi fulani, maana sasa hivi kila kitu kimepanda kuanzia vyakula hadi huduma za usafiri,” alisema.

Alisema kitendo hicho pia kitawaheshimisha watumishi kwa kuwa hapo zamani kazi ya utumishi, ilikuwa ikikimbiwa kutokana na mishahara kuwa midogo.

“Zamani utumishi ilikuwa inaonekana kama kujitolea, watu walikuwa wakikimbili sekta binafsi kwa sababu ya unafuu wa mishahara, lakini sasa Rais anaweka usawa katika ya sekta hizi mbili, ni jambo la kumshukuru,” alisema.

Rais alitoa ahadi ya nyongeza ya mshahara kwa watumishi katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) mwaka huu, ingawa si kwa kiwango walichokipendekeza 

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) cha Sh. milioni 1.01 kwa mwezi kwa sababu ya hali ya uchumi wa taifa na dunia siyo nzuri.

Juzi, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alinukuliwa na vyombo vya habari (si Nipashe) akimshukuru Rais Samia kwa kuwajali watumishi wa umma, kwa kuwa nyongeza hiyo italeta ahueni kubwa.

“Suala la nyongeza ya mishahara  tumelipokea vizuri kwa sababu ni ahadi yake ya Mei Mosi aliposema tuna jambo letu na tumpe muda wakaone watapandisha kiasi gani. Tunamshukuru kwa kutujali wafanyakazi, mwaka jana alipandisha madaraja na wengine mpaka leo wanaendelea kupanda madaraja,” alifafanua.

Imeandikwa: Jenifer Gilla na Beatrice Shayo

Habari Kubwa