Waeleza namna ya kumuenzi Nyerere

24Apr 2022
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Waeleza namna ya kumuenzi Nyerere

​​​​​​​VIONGOZI waandamizi wa serikali wamesema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwaunganisha Watanzania huku akichukia rushwa, ufisadi, uonevu, dhuluma na  ubaguzi.

Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere,

Wamesema katika kurithisha vizazi vijavyo falsafa zake, wazee na wanazuoni waendelee kuandika makala, majarida na vitabu kwa lengo la kuhakikisha urithi wa maisha yake unatambulika, kuhifadhiwa na kusherehekewa.

Wakizungumza jana katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mwalimu Nyerere yaliyoandaliwa na Mama Maria Nyerere nyumbani kwake, Msasani, Dar es Salaam, viongozi hao walieleza sababu ya kukumbukwa kwa kiongozi huyo.

Sherehe hizo zilibebwa na ujumbe usemao, ‘1922-2022 Ulikuwa Zawadi Kubwa Kwetu Familia, Taifa, Afrika na Ulimwengu.’

Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na viongozi wa serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), mabalozi, wapigania uhuru, wasomi, maofisa wa jeshi waliobeba jeneza la Hayati Mwalimu Nyerere na baadhi ya wafanyakazi wake wa wakati huo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema njia bora ya kumkumbuka Hayati Mwalimu Nyerere ni kutekeleza kwa vitendo urithi aliowaachia.

“Tutamkumbuka namna alivyojitoa muhanga kupigania ukombozi na ujenzi wa taifa hili kwa kushirikiana kwa pamoja na marehemu Amani Abeid Karume. Walisimamisha  nguzo imara za Muungano wetu ambao wiki ijayo (Aprili 26) tutasherehekea miaka 58 tangu kuasisiwa kwake,” alisema.

Dk. Mwinyi, alisema Hayati Mwalimu Nyerere katika kipindi chote cha uhai wake aliwaunganisha Watanzania akiamini umoja, upendo na mshikamano pamoja na kudumisha amani ni msingi muhimu na bora.

“Alichukia uonevu, dhuluma na ubaguzi wa kila aina, alichagua lugha ya Taifa letu kuwa ni Kiswahili akiamini kwamba ni lugha ya kutuunganisha na kutangaza utamaduni wetu.  Alitumia uhai wake kusisitiza umuhimu wa kuwa na siasa na mipango ya kujenga uchumi unaojitegemea na matumizi bora ya rasilimali,” alisema.

Pia alisema Mwalimu Nyerere aliamini umuhimu wa kuimarisha misingi ya utawala bora kwa kupiga vita rushwa, uzembe ufisadi wizi na ubadhirifu wa mali za umma na atakumbukwa kwa juhudi za kuongoza wapigania uhuru barani Afrika na kuimarisha umoja wa waafrika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa wito kwa wazee na wanazuoni kutumia njia za midahalo, mihadhara na wakati mwingine kuandika makala, majarida na vitabu kwa lengo la kuhakikisha urithi wa maisha ya Hayati Mwalimu Nyerere unatambulika, kuhifadhiwa na kusherehekewa.

Alisema matukio ya namna hiyo yatasaidia kuenzi, kuishi na kujirithisha falsafa ya Baba wa Taifa ambayo ni urithi na nguzo ya taifa ikiwa katika masuala yanayohusu maadili ya uongozi, muungano, dini, ukabila, na mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, alisema ofisi yake itaendelea kuhakikisha jukumu la ustawi wa viongozi wote waliostaafu akiwamo Maria Nyerere unaangaliwa vyema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alisema isingekuwa misingi imara aliyoiweka Hayati Mwalimu Nyerere ambayo ni amani, utulivu na kujitegemea basi wasingekuwapo hapo.

Anna Mwansasu ambaye amewahi kufanya kazi Ikulu na Butiama kwa Hayati Mwalimu Nyerere, alisema kabla ya kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere alipata bahati ya kwenda jijini London, Uingereza kumjulia hali na alipofika alimkuta Maria Nyerere anafuma.

“Nilipofika hospitalini Mwalimu Nyerere akaniambia: “Ninaumwa wameniambia itabidi waniongezee damu lakini wakiniongezea damu si itakuwa ya mzungu. Wakiniongezea  si nitakuwa siyo Kambarage tena? Pamoja na maumivu aliyokuwa nayo Mwalimu aliongea kwa utani kujitia moyo wa matumaini.”.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema chama kitaendelea kuzingatia misingi imara aliyowaachia Hayati Mwalimu Nyerere.

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba alisema Hayati Mwalimu Nyerere alipenda dini lakini alikwepa kuingiza siasa ndani yake, alikuwa mwadilifu, mwenye nidhamu ya hali ya juu, alikuwa na uongozi jumuishi na alipenda kusikiliza.

Mtoto wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara alisema: "Ninashukuru nimezaliwa na wazazi wema mmoja ametangulia mbele ya haki na mwingine bado yupo.”

Alisema: “Mgeni rasmi umezaliwa na wazazi wema Rais Mstaafu ni mtu mwema (Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi), ukiangalia mambo yako yamenyooka ila yangu yana mauzauza, huku ukubwani kuna marafiki tunakutana nao si watu wazuri. Ukiniona  ninamauzauza siyo ya Mwalimu Nyerere ni yangu mwenyewe”.

Katika sherehe hizo Mama Nyerere alitoa zawadi ya mbuzi kwa viongozi watano ambao ni Rais Samia, Rais Dk. Mwinyi, Majaliwa, Kinana na Majenerali wawili (Kidata na Kalembo) mbuzi mmoja.

Habari Kubwa