Wafanyabiashara 1,950 wapewa elimu ya kodi

28Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Iringa
Nipashe
Wafanyabiashara 1,950 wapewa elimu ya kodi

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewafikia wafanyabiashara 1,950 wa Mkoa wa Iringa wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyofanyika kuanzia Februari 17 hadi 27, mwaka huu.

Kampeni hiyo ni kwa ajili ya kuwaelimisha baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya za Kilolo, Manispaa ya Iringa na Mufindi.

Akizungumza baada ya kuhitimisha kampeni hiyo mkoani humo, Ofisa Msimamizi wa Kodi Mwandamizi wa TRA, Catherine Mwakilagala, alisema kampeni hiyo imeleta mafanikio makubwa kwa kuwafikia na kuelimisha idadi hiyo ya wafanyabiashara.

“Mamlaka ya Mapato Tanzania tumehitimisha kampeni ya elimu kwa mlipakodi katika mkoa huu wa Iringa na kampeni hii imefanikiwa sana kwa sababu tumewafikia walipakodi 1,950 ambao wote tumewapatia elimu ya kodi na wamepata nafasi ya kutoa maoni na changamoto zao ambazo tumezipokea na nyingine tumezipatia ufumbuzi,” alisema Mwakilagala.

Meneja wa TRA mkoani humo, Lamson Tulyanje, alitoa wito kwa wafanyabiashara wote waliotembelewa na maofisa wa TRA kwenye maduka yao na waliopata elimu kupitia semina wakati wa kampeni hiyo, kutumia elimu waliyoipata kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati na hiari.

“Elimu ambayo wameipata wafanyabiashara mbalimbali kwenye kampeni hii ya elimu kwa mlipakodi, ni vizuri waitumie katika kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati ili serikali iweze kutimiza majukumu yake ya kuwapatia huduma mbalimbali wananchi,” alisema Tulyanje.

Richard Kilawa, mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi kutoka Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani humo aliishukuru TRA kwa kumfikishia elimu ya kodi dukani kwake na aliahidi kuendelea kulipa kodi kwa hiari.

“Ninashukuru sana TRA kunitembelea dukani kwangu na elimu yao imenifundisha kulipa kodi kwa hiari. Hivyo, nitawashawishi wafanyabiashara wenzangu walipe kodi kwa hiari ili tujenge nchi yetu,” alisema Kilawa.

Naye mfanyabiashara wa mbao wa halmashauri hiyo, Maura Ng’umbi, alisema kupitia elimu iliyotolewa na maofisa wa TRA wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi, imemsaidia kujua umuhimu wa kulipa kodi stahiki kwa manufaa ya taifa.

Habari Kubwa