Wafanyabiashara 600 soko la Ilala hatarini

11Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wafanyabiashara 600 soko la Ilala hatarini

WAFANYABIASHARA 630 katika soko la Ilala jijini Dar es Salaam, wapo hatarini kupoteza maisha kama mvua zitanyesha kutokana na jengo wanalotumia paa lake lilioezekwa kwa zege, kuharibika vibaya.

Wafanyabiashara watakaokutwa na zahama hiyo ni mamalishe 300 na mafundi cherehani 330 huku jengo hilo likikosa madirisha, kutanda giza na wanatumia vibatari mchana kutokana na mfumo wa umeme kuharibiwa na uchakavu.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa muda wa wiki mbili, umebaini moja ya paa kubwa lililoezekwa kwa zege kuanza kuanza kuvuja na kutiririsha maji na wakati huo wafanyabiashara wakitumia turubai na kuendelea kufanya shughuli zao.

Katibu wa mafundi cherehani ,Hamis Siogopi, alisema amekuwa akifanya biashara kwenye soko hilo kwa zaidi ya miaka 20 na kwamba uharibifu wa sasa unaonyesha hatari kubwa tofauti na miaka ya nyuma.

“Ni kweli maisha yetu yapo hatarini mno, lakini hatuna la kufanya na soko hili ni ndogo, hakuna sehemu ya kuhamia tukiondoka sehemu hii tutaishije na familia zetu?” alihoji.

Alisema viongozi wengi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, akiwamo Mkurugenzi wamewahi kuwatembelea na kujionea hatari na waliishia kuahidi kuwapatia sehemu nyingine ili wabomoe jengo hilo, lakini hawajatimiza ahadi hizo kwa miaka mingi.

Swaumu Hassani, mamalishe, alisema wanaishi maisha magumu kutokana miundo mbinu ya jengo hilo kuharibika vibaya ikiwamo mifereji ya kutirirsha maji nje kuziba na kulazimika kutumia ndoo.

“Hili giza limetuathiri maana wateja wengi wanaogopa kuingia ndani kula chakula badala yake wanataka tuwapelekee kule waliko,” alisema akionekana kukata tamaa.

Swaumu alisema wakati wa mvua hali inakuwa mbaya kutokana na vibatari kuzima na majiko kulowa maji kutokana na kila mtu kukimbizia jiko sehemu moja ambayo ni ndogo,

Aliongeza: “Hapa hatuwezi kuhama,maana kuna wakati uongozi wa soko uliamuru tuondoke wafanye ukarabati, tuliondoka miezi miwili, lakini hakuna kilichofanyika ikabidi turudi.”

Alisema ushuru wanaotozwa kwa siku wa Sh. 1,000 ni mkubwa sana wakati wauza mitumba ni Sh. 500, hivyo wanaiomba serikali iwaangalie kama walipakodi kubwa.

Mwenyekiti wa soko la Ilala, Issa Malisa, alisema soko hilo lina changamoto nyingi, ukiwamo mfumo wa kupeleka maji kuziba.

Alisema kuwa uongozi wa Manispaa hausikilizi kilio cha wafanyabiashara hao na kwamba zimeandikwa barua nyingi za kuomba msaada wa kufunika mitaro ili kuokoa maisha ya wafanyabiashara na umma kwa ujumla, lakini zimekwamishwa kwa ahadi zisizotekelezwa.

Ofisa wa Soko kutoka Manispaa hiyo, Jastinne Chasama, alisema tuhuma hizo ni za kweli, lakini tatizo kubwa soko hilo limezidiwa na wafanyabiashara ambao walitakiwa wawe 800, lakini kwa sasa wako 36,000.

Alifafanua kuwa wafanyabiashara walitakiwa kuondoka ili ukarabati ufanyike, lakini walipoona bajeti imechelewa kupitishwa, walirudi na kwa sasa hawawezi kuwaondoa.

Alisema kuwa bajeti inayotakiwa kupitishwa ili ukarabati wa soko uanze ni Sh. milioni 400.

Habari Kubwa