Wafanyakazi 15,000 kunufaika ajira mradi wa SGR

31Jan 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe Jumapili
Wafanyakazi 15,000 kunufaika ajira mradi wa SGR

WAFANYAKAZI 15,000 watarajia kunufaika na ajira katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa wakati wa kongamano la mpango Kazi na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa(SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka  iliyofanyika  jana katika mkoani Mwanza.

Mhandisi Kadogosa alisema mradi huo utakaoigharimu serikali fedha sh Trilioni 3 utatoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira rasmi kwa wafanyakazi 15,000 huku wafanyakazi wengine 75,000wakipewa ajira za muda mfupi.

Kadogosa alisema faida nyingine ya ujenzi wa mradi huo ni pamoja na kuzalisha zabuni mbalimbali za usafirishaji, usambazaji wa vifaa vya ujenzi pamoja na kutoa fursa kwa wakandarasi mbalimbali  wa makampuni ya ukandarasi ili kuwajengea uwezo wa kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa.

"Ili Tanzania iwe ya viwanda lazima iwe na reli imara hivyo agizo la utekelezaji wa mradi huo ni la Rais Magufuli likiwa na sababu za msingi za kukidhi matakwa ya makubaliano ya kimkakati ,uhusishwaji wa kiteknolojia, kujiandaa na kujenga uwezo wa sisi kuweza kujenga " alieleza Kadogosa. 

Akizungumzia suala la vishoka wanaoibuka wakati wa utekelezaji wa miradi alisema watawaondoa kwa ushirikiano na sekta binafsi kwa sababu wanahitaji watu wanaofanya kazi kwa umakini.

Akifungua kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella aliwahakikishia usalama wa kutosha  wakati wa ujenzi huo na kusaidia upatikanaji na utatuzi wa changamoto kwa wale wataokuwa na tatizo.

Alisema bado wanatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa meli, daraja la Magufuli na ukarabati wa uwanja wa ndege hivyo kwa mradi wa reli kila mtu aingie kwenye mfumo wa kufuata utaratibu na ueledi katika utendaji kazi.

Alisema katika miezi 36 ya utekelezaji huo wadau mbalimbali na wananchi waione ni fursa na kufatilia namna watakavyoweza kuwekeza mkoani humo.

Mkandarasi Mkuu wa Kampuni ya China Civil Engineering construction Company inayojega mradi huo Junle Zhang alisema watatekeleza mradi huo kwa ueledi na watahakikisha kuwa wanaukamilisha ndani ya muda uliopangwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF  Fransis Nanai amewataka wadau wote ikiwemo walioshiriki kongamano hilo kuchangamkia fursa katika ujenzi wa mradi huo ili kunufaika na fedha zaidi ya sh Trilioni 1 Kati ya trillion 3 za mradi zinazotazamiwa kubaki nchini.

Naye Meneja wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Machibya Masanja alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa safari kutoka Mwanza hadi Isaka na kurahisisha ubebaji wa mizigo mikubwa kwa wakati mmoja kwa umbali wa kilomita 341.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA Dkt Jacqueline Mkindi alisema sekta ya kilimo inaumuhimu katika maendeleo ya nchi hivyo harakati mbalimbali zitafanyika ili kuchukua fursa zilizopo katika sekta hiyo pamoja na masoko ya ndani na ya kanda yaliyopo wanatakiwa kutambua namna ya kuyafikia.

Alisema Tanzania imekaa kimkakati wa kuweza kuuza mazao kwa nchi yeyote duniani hivyo aliwaomba wadau wa kilimo kuwa pamoja na kujenga umoja wenye tija ili kuweza kupata fursa zitakazowanufaisha.

Habari Kubwa