Wafanyakazi wazidi kulia makali ya kodi ya mshahara

09Mar 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wafanyakazi wazidi kulia makali ya kodi ya mshahara

WAKATI serikali ikiendelea na maandalizi ya bajeti ya mwaka 2019/20, Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), kimetoa mapendekezo mbalimbali ikiwamo kufanyika mapitio ya makato ya kodi ya mshahara (PAYE) ili kutoa nafuu kwa mfanyakazi.

Mwenyekiti wa THTU, Dk. Paul Loisulie, picha augusta njoji

Mapendekezo hayo yalitolewa jana na Mwenyekiti wa THTU, Dk. Paul Loisulie, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa baada ya chama hicho kupitia kamati ya uchambuzi na ushauri kuandaa mapendekezo kuhusu bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema katika bajeti ijayo, wanashauri yafanyike mapitio katika viwango vya kodi vya mtu binafsi inayohusiana na PAYE ili kumpatia mfanyakazi unafuu wa kodi.

“Mapendekezo yamezingatia mfumo wa kodi wa nchi zingine za Afrika Mashariki na kusini mwa jangwa la Sahara na pendekezo mahususi linalotolewa ni kupandisha kima cha chini kisichokatwa kodi kutoka Sh. 170,000 hadi Sh. 360,000, hatua ambayo itapunguza maumivu ya kodi kwa mfanyakazi,” alisema.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, katika kima cha chini cha mapato yasiyozidi Sh. 170,000  hakuna kodi inayokatwa, lakini mapato yanayozidi kiwango hicho hadi Sh. 360,000 kodi inayokatwa ni asilimia tisa.

Pia alisema mapato yanayozidi Sh.360, 000 hadi Sh.540, 000 kiasi kinachokatwa ni Sh.17, 100 pamoja na asilimia 20 ya mapato yanayozidi kiasi hicho.

Aidha, alisema kwa mapato yanayozidi Sh. 540,000 hadi Sh.720, 000 kiwango cha kodi kinachokatwa ni Sh.53, 100 jumlisha asilimia 25 ya mapato yanayozidi Sh. 540,000 na Sh. 98,100 jumlisha asilimia 30 ya mapato yanayozidi Sh.720, 000.

Alisema kwa sasa hawajazungumzia suala la kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa kuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limeshafanya wajibu huo ambao wanaunga mkono.

“Mapendekezo haya ni muhimu kwa ajili ya kuleta unafuu wa kodi kwa mfanyakazi bila kubadili viwango vya asilimia vilivyopo kwa sasa, maana asilimia imeshuka hadi tisa lakini haijaleta nafuu kwa mfanyakazi,” alisema.

Alifafanua kuwa serikali imeendelea kuahidi namna nzuri ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kulingana na uwezo wa mapato yake kwa lengo la kuwawezesha kumudu gharama za maisha.

“Maeneo ambayo yamekuwa yakitiliwa mkazo ni pamoja na ongezeko la mshahara hasa kima cha chini, kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwenye mishahara, malipo ya mshahara kwa wakati, kuwapandisha vyeo watumishi, kulipa malimbikizo ya mdai ya watumishi na kuhakikisha watumishi wanalipwa mafao yao mara baada ya kustaafu,” alisema.

Hata hivyo, alisema suala la kuboresha maslahi ya watumishi halijafanyika na kupewa uzito unaostahili katika bajeti za serikali hivyo kuwafanya watumishi kufanya kazi katika mazingira magumu na kuishi maisha yasiyo na staha na kuathiri utendaji wao wa kazi.

“Suala la upandishwaji wa madaraja, nyongeza ya mwaka ya mshahara na malipo ya posho kwa watumishi limekuwa gumu kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hivyo kuchangia malalamiko kutokana na ulimbikizwaji wa madai ya wafanyakazi na kuwafanya wabakie katika kipato au madaraja yale yale kwa muda mrefu,” alisema.

Dk. Loisulie alisema kodi inayotokana na mishahara PAYE ndio chanzo kikubwa na imara kwenye vyanzo vya mapato ya serikali.

MAPENDEKEZO MENGINE

Mbali na kodi, alisema THTU inaomba serikali iangalie uwezekano kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 kuweka utaratibu wa kulipa madeni ya ndani na nje pamoja na madeni ya makandarasi wa ndani, malimbikizo ya stahiki mbalimbali ya wafanyakazi wa umma.

“Inashauriwa ukopaji utakaofanyika kwa mwaka wa fedha 2019/20 uwe kwa ajili ya miradi ya maendeleo na inayoleta tija kwa taifa,” alisema.

Pia alisema wanapendekeza sekta zilizopewa kipaumbele kwa mwaka huo ni pamoja na miradi ya umeme inayotumia mfumo wa maji, ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa, barabara na ukuaji wa sekta ya anga.

“Lengo kuu ni kurahisisha na kuhamasisha ukuaji wa sekta ya utalii hasa nje ya mipaka ya Tanzania, ingawa katika bajeti ya mwaka 2019/20 serikali imeweka mkazo katika kuboresha miundombinu itakayovutia uwekezaji nchini, suala la kutoweka vipaumbele katika sekta za huduma za kijamii pamoja na kilimo zinatia shaka juu ya hatua madhubuti zinazochukuliwa katika kuboresha maisha ya watu, wakiwamo wakulima na wafanyakazi,” alisema.

Kadhalika, alisema ili kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, sera za mapato kwa mwaka wa fedha 2019/20 zijikite katika kuongeza na kuboresha wigo wa kodi na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato, kuimarisha usimamizi wa vyanzo vilivyopo hususan katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki na hatua nyingine za kiutawala na kupunguza matumizi yasiyo na tija.

MAENEO YA KUONGEZA KODI

Alisema kuendelea kurasimisha sekta zisizo rasmi na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kupata vyanzo vipya vya mapato, mfano uthaminishaji wa majengo na kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi, kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wadogo wadogo kama Machinga, wavuvi, shughuli za ufundi , ujenzi, useremala, uchomeleaji, washonaji na mama lishe.

“Wachomaji wa nyimbo kwenye CD na flash ili kulinda kazi za wasanii nao usisahaulike katika kutozwa kodi, Mifumo ya kielektroniki itasaidia kuwatambua na kutengeneza utaratibu rafiki wa kutoza kodi,”alisema.

Alisema michezo ya kamari na kubahatisha kuongezewa kiwango cha kodi ambapo wanapendekeza ongezeko la kutoka asilimia 18 hadi 30 .

“Serikali ya Kenya yenyewe inatoza asilimia 35 ya pato ghafi, hii itasaidia pia kuondoa urahibu kwa vijana na kuelekeza nguvu kwenye shughuli zingine za kimaendeleo,”alisema.

Vilevile alisema misamaha ya kodi itathiminiwe, isiyo na tija ipunguzwe zaidi ili kuongeza makusanyo ya serikali.

“Tunatambua umuhimu wa misamaha ya kodi katika kuchochea maendeleo, hasa maendeleo ya jamii na uwekezaji. Lakini pia wanufaikaji wanatumia vibaya misamaha hiyo kwa maslahi binafsi na kuipotezea serikali mapato, tunashauri kuwapo na umakini na ufuatiliaji wa kina kwenye misamaha hiyo, ili itumike kama ilivyokusudiwa na sio kutumika kwa manufaa binafsi, ikumbukwe Tanzania imeonekana ina misamaha ya kodi mingi kuliko nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema.

Alisema pia Ofisi ya Msajili wa Hazina iimarishe usimamizi na ukaguzi kwenye kampuni ambazo serikali ina hisa ili kuhakikisha kuwa gawio stahiki katika uwekezaji wake linapatikana.

“Mamlaka za Serikali za Mitaa zijielekeze kwenye miradi itakayochochea upatikanaji wa mapato katika mamlaka hizo hususan viwanda, minada ya mifugo, masoko na machinjio ya kisasa, stendi za mabasi, stendi za maegesho ya malori, ushuru wa mazao na maghala ya kuhifadhia nafaka. Utekelezaji wa haya utapunguza utegemezi kwa serikali kuu,”alisema.

Alishauri Maafisa Masuhuli wazidi kusisitizwa kutumia makandarasi na watoa huduma wanaotumia mashine za kielektroniki za kukusanya mapato na ambao wanakumbukumbu safi za kulipa kodi kutoka TRA.

LESENI YA UDEREVA

Alisema wanapendekeza ongezeko la kodi, vyanzo vipya baadhi ya maeneo ikiwamo kwenye leseni kutoka Sh.40,000 hadi Sh.50,000 za udereva, leseni ya majaribio iwe Sh.10,000.

Habari Kubwa