Wafanyiwa upasuaji bila kufungua vifua

08Oct 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Wafanyiwa upasuaji bila kufungua vifua

WATOTO 28 waliozaliwa na maradhi mbalimbali ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kati ya hao 19 wamefanyiwa operesheni bila kuhusisha upasuaji wa kifua.

Kwa mujibu wa taarifa yao iliyotolewa jana na taasisi hiyo, ni watoto tisa kati ya hao ndio waliofanyiwa operesheni iliyohusisha ufunguaji wa kifua.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa JKCI, Naiz Majani, alisema katika taarifa hiyo kuwa upasuaji huo ulianza kufanyika hospitalini hapo mwanzoni mwa wiki hii na ulitarajiwa kukamilika jana.

Dk. Majani alisema upasuaji huo umefanyika kwa kushirikiana na madaktari wenzao bingwa kutoka shirika la Kimarekani la Mending Kids International.

Aidha, alisema huduma za matibabu ya moyo zilianza rasmi kutolewa nchini mwaka 2008 na hadi mwaka 2015, watoto 200 walifanyiwa upasuaji huo.

“Lakini mwaka 2015 tuliona vyema kuanzisha kitengo maalumu cha upasuaji kwa ajili ya watoto. Hadi kufikia mwaka huu, tumewafanyia upasuaji zaidi ya watoto 500. Hiyo ni ndani ya kipindi cha miaka miwili pekee,” alisema.

Dk. Majani alisema ni manufaa makubwa kuanzishwa kwa kitengo hicho kwa sababu kimeokoa maisha ya watoto wengi.

“Kwa mwaka serikali ilikuwa na uwezo wa kupeleka nje ya nchi watoto 40 hadi 80 kupatiwa matibabu haya,” alisema na kuongeza kuwa watoto  wengine 145  wanasubiri huduma ya upasuaji.